Saudia yazuia kombora kutoka Yemen
5 Januari 2018Katika taarifa, jeshi la Saudi Arabia linaloongoza muungano wa majeshi yanayopambana na waasi nchini Yemen imesema ulinzi wa anga wa nchi hiyo umelizuia kombora hilo na kwamba hakuna majeruhi ya aina yoyote.
Wahouthi ambao wako katika mapigano na serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudi Arabia, mapema walisema kwamba walikuwa wamerusha kombora katika mji wa kusini mwa Saudia wa Najran.
Shambulizi lililenga maeneoe yenye idadi kubwa ya watu
Saudi Arabia inayoongozwa na Wasunni imeituhumu Iran mara kwa mara kwa kuwapa silaha Wahouthi ingawa Iran inakanusha tuhuma hizo na msemaji wa muungano wa majeshi yanayoongozwa na Saudi ArabiaTurki al-Maliki anasema shambulizi hilo la Wahouthi ni ishara ya Iran kuwaunga mkono.
Maliki amesema pia kwamba shambulizi hilo lilikuwa linalenga maeneo yaliyo na idadi kubwa ya watu na kwamba lilisababisha uharibifu mdogo katika mali ya raia mmoja wa Saudia Arabia.
Marekani ambayo ni rafiki wa muda mrefu wa Saudi Arabia imesema kwamba Iran ilitengeneza kombora ambalo lilirushwa na Wahouthi katika uwanja wa ndege wa Riyadh mwezi Novemba.
Mwezi Desemba Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley aliwasilisha kile alichokitaja kuwa ushahidi kwamba kombora hilo lilikuwa limetengenezwa na Iran. Iran ilikanusha na kusema kwamba ushahidi huo umebuniwa tu.
Wahouthi wamezidisha mashambulizi dhidi ya Saudia tangu Novemba
Ripoti moja iliyowasilishwa mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Desemba ilisema kwamba maafisa wa Umoja huo wa Mataifa walichunguza vifusi vilivyotokana na kombora hilo lililorushwa Saudi Arabia na wakapata kwamba lilitengenezwa na nchi wanayoijua ingawa hawakuweza kuthibitisha kwamba ni Iran.
Wahouthi wamezidisha mashambulizi ya roketi dhidi ya Saudi Arabia tangu mwezi Novemba.
Muungano wa majeshi unaoongozwa na Saudi Arabia uliungana na serikali ya Yemen mwezi machi mwaka 2015 baada ya waasi kuuteka Mji Mkuu wa nchi hiyo Sanaa. Licha ya nguvu ya muungano huo wa majeshi, waasi bado wanaudhibiti Mji huo Mkuu na sehemu kubwa ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Kulingana na shirika la afya duniani WHO watu 8,750 wamefariki dunia tangu jeshi hilo liingie nchini Yemen. Nchi hiyo pia kwa sasa inakabiliwa na kile ambacho Umoja wa Mataifa umekiita mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu.
Mwandishi: Jacob Safari/AFPE
Mhariri: Gakuba Daniel