Sauti za Deutsche Welle
17 Januari 2013 Tuliisubiri sana, tuliona yachelewa
Sasa ‘mefika salama, bila hata kupwelewa
Siku hii ya kufana, Deutsche Welle kuzaliwa
Kwa kuzaliwa mwana, vizuri amelelewa
Radio yetu mahiri, hamsini kufikia
Ni miaka ya habari, sisi tunaosikia
Twajionea fahari, myaka hii kuwadia
Yawe maisha mazuri, sisi tunawaombea
Watangazaji wazuri, wote tunawakubali
Tena walio mahiri, wapo hapo Deutsche Welle
Salma wa Zanzibari, leo twakupa kibali
Sauti yako hatari, kama mramba asali
Leila Ndinda Uganda, dada nakupa hongera
Sana mimi nakupenda, sauti yako yang’ara
Hata boti unapanda, kama unatoka Ngara
Kazi yako waipenda, kweli wewe ni kinara
Nawe Saumu Mwasimba, heko pia tunakupa
Kakujalia Muumba, kwa kipaji alokupa
Sauti unaipamba, na hutangazi kwa pupa
Unajua kujiremba, na saluti ninakupa
Mkono tunaupunga, kwako Kitojo wa Seki
Twakusalimu Lusanga, ingawa kuja hutaki
Tukisikia twaringa, twakuona kama keki
Sauti isiyo chenga, tulivu tumehakiki
Dada Grace wa Kabogo, wa boni Ujerumani
Siku uje kwetu Bongo, kukuona natamani
Japo ukae kidogo, au mimi nije Boni?
Mnipe nafasi ndogo, nitembee Ujerumani
Hamida Issa na Umi, na Hawra wa Shamte
Mnatangaza kisomi, tunawasikia kote
Ninawapendaje mimi? Na wasikilizaji wote
Sauti kama sunami, zaenea anga lote
Dar es Salaam Njogopa, kaka ninakupa tano
Kazi bila kuogopa, huhitaji malumbano
Wengi pongezi twakupa, wazi bila minong’ono
Vikwazo unavichupa, ulegevu kwako no!
Amina Abubakari, natamani kukuona
Sauti yako nzuri, nione ‘navyofanana
Mtangazaji mahiri, sote twakubaliana
Usomaji wa habari, unaupatia sana
Jamani wa Deutsche Welle, Bonn ya Ujerumani
Sisi tunavyowajali, myaka hii hamsini
Tena tunawakubali, mko mbali kileleni
Mko juu tena mbali, hakuna ulimwenguni
Mimi naitwa Ginzera, baba yangu nduye Juma
Mimi ni mama imara, nipendaye kujituma
Darisalama Kimara, maisha nimeyafuma
Naishi maisha bora, Mungu kanipa salama
Tanbihi: Shairi hili limeandikwa na Bi Ginzera Juma wa Kimara, Dar es Salaam - Tanzania, na picha imechorwa na Fredrick Yustard Ngimbwa wa Dar es Salam, Tanzania kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya Idhaa ya Kiswahili ya DW.
Mhariri: Mohammed Khelef