Scalise hajathibitisha uungwaji mkono unaohitajika
12 Oktoba 2023Siku moja baada ya kumshinda mwenyekiti wa kamati ya bunge ya haki na sheria Jim Jordan katika uteuzi huo wa chama cha Republican kugombea wadhifa wa Spika wa bunge la Marekani, Scalise, mbunge wa Louisiana alikuwa bado hajathibitisha kama angeweza kupata kura 217 za chama hicho zinazohitajika kuvuka vihunzi vya upinzani wa chama cha Demokratic na kuchaguliwa katika wadhifa huo wenye ushawishi mkubwa.
Scalize asema kuna kazi kubwa ya kufanywa
Baada ya uteuzi wake wa jana, Scalize alisema kwamba ni wazi kwamba bado wana kazi ya kufanya sio tu katika bunge kwa manufaa ya watu wa nchi hiyo , lakini kutokana na jinsi ulimwengu ulivyo hatari na jinsi mambo yanaweza kubadilika haraka sana.
Soma pia: Kevin McCarthy aondolewa kama Spika wa Bunge la Marekani
Mbunge wa chama cha Republican John Duarte anayemuunga mkono Scalise, amesema watakapoenda bungeni,
kutakuwa na angalau matarajio makubwa kwa upande wa Scalise na timu yake kwamba ana uungwaji mkono.
Kura ya chama cha Republican yakosa kupigwa
Awali wabunge wa chama cha Republican walikuwa wamepanga mkutano wa chama hicho hapo jana alasiri iwapo Scalise atapata haraka uungwaji mkono wa uchaguzi huo, lakini hakuna kura iliyopigwa. Chanzo kilichozungumza kwa sharti la kutotambulishwa, kimesema kuwa Jordan alipanga kumpigia kura Scalise na kuwahimiza wabunge wenzake wa chama cha Republican kufanya hivyo pia.
Hali ya sintofahamu ililighubika bunge hilo zaidi ya wiki moja baada ya wabunge wanane wa chama cha Republican kuchangia kumuondoa madarakani aliyekuwa Spika wa bunge hilo McCarthy kwa usaidizi wa wabunge wa chama cha Democratic, huku baadhi ya wabunge wakiwa bado wanamuunga mkono hadharani Jordan na wengine wakiapa kumpigia kura McCarthy.
Soma pia:
Huku McCarthy akiwa spika wa kwanza kuondoloewa kwa kura rasmi, maspika wawili wa mwisho wa chama cha Republican kushikilia wadhifa huo, waliuachia baada ya shinikizo kutoka kwa wanachama wenye misimamo mikali.
Warepublican waazimia kuepuka kujirudia kwa tukio la aibu
Warepublican wameazimia kuepuka kujirudia kwa tukio la aibu la umma lililotokea mnamo mwezi Januari, wakati wanachama wenye misimamo mikali wa chama cha Conservative walipomfanya McCarthy kupgiwa kura mara 15 bungeni kwa muda siku nne kabla ya kushinda wadhifa huo.
Lakini wasiwasi huo unaonekana kutokuwa na ushawishi wa kutosha kuleta umoja faraghani, huku zaidi ya wabunge kumi na wawili wakiwa aidha hawajafanya maamuzi ama wanampinga Scalise.