Schalke 04 bado matokeo ni mabaya
26 Septemba 2016Schalke 04 imeshindwa kwa mara ya nne kupata ushindi katika Bundesliga msimu huu baada ya kupoteza mchezo wake jana jumapili dhidi ya Hoffenheim kwa mabao 2-1. Hoffenheim imepata ushindi wake wa kwanza katika msimu huu baada ya sare nne mfululizo wakati Lukas Rupp alipofunga bao katika dakika ya 41. Mapema Andrej Kramaric alisawazisha bao lililofungwa na Eric Maxim Choupo-Moting katika dakika ya nne kwa Schalke.
Nahodha wa Schalke Benedict Howedes alikuwa na haya ya kusema:
"Kwa kweli tulianza vizuri . Tulipata bao zuri kabisa. Hata hivyo baadaye tulianza kujilinda na katika hali hii hatukuwa maini sana. Tunafungwa mabao mengi ambayo ni kwa njia rahisi sna. Nashindwa kuelewa , ni vipi tunaweza kufungwa mabao kama hayo. Na hapa kwa mara nyingine tena tumeshindwa mchezo ambao hatukupaswa kushindwa, na hii inauma sana."
Mbali ya kupata mapokezi mabaya mjini Kolon , lakini wageni katika ligi ya Bundesliga RB Leipzig walipata sare muhimu kwao , wakati timu zote hizo zikibakia bila kushindwa katika mchezo wa tano wa msimu huu, baada ya kutoka sare kwa bao 1-1.
Mashabiki wa FC Kolon walilizuwia basi lililokuwa likiwaleta wachezaji wa Leipzig na mchezo ulianza dakika 15 baada ya muda uliopangwa. Leipzig inafadhiliwa na kampuni ya Austria inayotengeneza kinywaji baridi cha kutia nguvu na kuchipuka kutoka katika ligi za chini hadi katika Bundesliga msimu huu. Mashabiki wengi wa Bundesliga hawafurahishwi na kikosi hicho kutokana na mahusiano yake ya kibiashara na kampuni hiyo. Mchezaji aliyesainiwa msimu huu na Leipzig , raia wa scottland Oliver Burke, alicheza kwa mara ya kwanza na alipachika bao katika dakika ya tano ya mchezo. Kolon walisawazisha katika dakika ya 25 kwa bao la yuya Osako.
Huyu hapa Marcel Sabitzer wa RB Leipzig .
"Nafikiri katika kipindi cha kwanza tulianza vizuri. Tuliweza kupata bao. Na baada ya hapo tulicheza vizuri. Lakini Kolon waliweza kurejesha bao haraka. Na baada ya hapo wwalicheza vizuri pia. Katika kipindi cha pili timu zote hazikuweza kucheza vizuri kutokana na kuchoka kwasababu ya michezo mfululizo. Tulijaribu kila kitu, lakini tunafuraha kupata pointi moja kutoka hapa."
Hadi sasa Bayern Munich inaongoza Bundesliga kwa kuwa na pointi 15 , ambapo imeshinda michezo yake yote. Inafuatiwa na Borussia Dortmund katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 12, pamoja na FC Kolon ambayo ina pointi 11 katika nafasi ya tatu.
Kibarua chaota majani
Bayern iliishinda Hamburg SV kwa taabu siku ya Jumamosi kwa bao 1-0 lililofungwa katika dakika ya 91 na Joshua Kimmich, lakini hali ya ukakamavu iliyooneshwa na Hamburg haikuweza kumuokoa kocha Bruno Labbadia kung'olewa katika kiti chake kilichokuwa kinalegalega.
Ni mara ya pili katika msimu huu kushuhudia kocha kibarua kikiota majani, ambapo baada ya Werder Bremen kuachana na kocha wake Viktor Skriptnik wiki moja iliyopita, wiki hii Hamburg SV iliachana na kocha wake Bruno Labbadia Jana Jumapili jioni na kumtaja mrithi wake kuwa ni kocha wa zamani wa Hoffenheim Markus Gisdol na kusaini mkatab hadi Julai 2017. Gisdol mwenye umri wa miaka 47 pamoja na kocha wake msaidizi Frank Fröhling na Frank Kaspari wanatarajiwa kuanza rasmi kazi ya kuifunza Hamburg leo jioni.
Gisdol ambaye alifanyakazi na Hoffenheim tangu Aprili 2 , 2013 hadi Oktoba 26 , 2015 , alifanikiwa kuwaweka Kevin Volland, Sebastian rudy na Roberto Firmino ambaye hivi sasa yuko na Liverpool kuwa wachezaji wa timu za taifa za Ujerumani na Brazil.
Matarajio ya Hamburg kwa Gisdol ni kuiondoa timu hiyo kutoka mkiano mwa ligi, na pia kuipa makali safu ya ushambuliaji ambapo wachezaji kama Boby Wood na Filip Kostic wameshindwa kuzifumania nyavu za maadui chini ya uongozi wa Labbadia.
Katika ligi ya Uingereza Premier League , Manchester United iliondoka kifua mbele mbele ya mabingwa watetezi Leicester City siku ya Jumamosi kwa kuizaba mabao 4-1 ambapo kocha wa Jose Mourinho aliweka kando kutokuwapo uwanjani kwa Wayne Rooney kuwa ndio sababu ya kikosi chake kufanikiwa kutandaza kandanda safi siku hiyo na kuudhibiti mchezo. Mourinho alisema.
"Leo ilikuwa muhimu kuwa na watu wenye kasi uwanjani kupambana na timu ambayo inashambulia kwa kushitukiza moja kwa moja kuanzia katika robo ya eneo lao wakipiga mipira ya mbali na wachezaji kufikia mara mpira unapotua upande wa pili. Kwa hiyo tumebadilisha timu kucheza dhidi ya Leicester kwa kuwa na uwezo maalum walionao".
Chelsea ilikiona cha mtema kuni baada ya kufanya makosa makubwa kila mara katika ulinzi na kuzabwa mabao 3-0 na Arsenal London wakati kikosi cha mzee Arsene Wenger kilifikisha mwisho ukame wa mabao katika michezo sita ya ligi dhidi ya majirani zao hao mjini London kwa kupachika mabao 3 katika kipindi cha kwanza.
Liverpool haijatawazwa mabingwa wa England tangu mwaka 1990 na mchezo dhidi ya Hull City umejionesha kwamba timu hiyo inarejea katika safu yake tena.
Manchester City wanaongoza ligi hiyo kwa kushinda michezo yake yote sita na Jumamosi iliizaba Swansea City kwa mabao 3-1.
Bayern Munich, Borussia Dortmund na Borussia Moenchengladbach zinakabiliana na changamoto kutoka Uhispania katika Champions League wiki hii wakati Bundesliga inajipima nguvu dhidi ya vilabu kutoka La Liga , Premira Division.
Borussia Dortmund itakuwa wenyeji wa mabingwa watetezi Real Madrid kesho Jumanne wakati siku ya Jumatano itakuwa zamu ya Gladbach kuoneshana kazi na FC Barcelona na Bayern Munich inajaribu kulipa kisasi cha kuondolewa katika nusu fainali mwaka 2016 na atletico Madrid.
Mara hii Bayern Munich iko chini ya ukufunzi wa kocha mpya Carlo Ancelotti ambaye ameonesha uwezo mkubwa kwa kushinda hadi sasa michezo yote mitano katika Bundesliga.
"Tumecheza na timu za Uhispania katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na kila wakati tulishindwa", amesema mwenyekiti wa Bayern Karl-Heinz Rummenigge. Tukiwa na kocha Carlo Ancelotti tunataka kuwaonesha Atletico Madrid kwamba tunaweza kushinda hata pointi moja ama tatu kwao." ameongeza Rummenigge.
Michezo mingine ni kati ya Monaco ikikwaana na Bayer Leverkusen ya Ujerumani , CSKA Moscow ikioneshana kazi na Tottenham Hotspurs ya Uingereza , Sporting Lisbon ina miadi nyumbani na Legia Warsaw, Club Brugge inasafiri kwenda kwa FC Copenhagen ya Denmark , wakati Leicester City mabingwa wa Uingereza wako nyumbani wakiisubiri FC Porto ya Ureno.
Champions League Afrika
Na katika bara la Afrika Zamalek ya Misri ilipata kipigo cha mbwa mwizi cha mabao 5-2 mbele ya wababe wa Morocco Wydad Casablanca siku ya Jumatatu lakini walihimili kishindo hicho na kufanikiwa kufuzu kukutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika kusini katika fainali ya kombe la Champions League barani Afrika.
Mabingwa hao mara tano wa Afrika walishinda mchezo wao wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali kwa mabao 4-0 mjini Alexandia mwishoni mwa juma lililopita na kufanikiwa kujipenyeza katika fainali kwa jumla ya mabao 6-5.
Ikijaribu kuwa timu ya kwanza kufuta kipigo cha mabao manne katika nusu fainali, ya kombe la champions league barani Afrika , Wydad ilikuwa inaongoza kwa mabao 5-1 dakika 26 kabla ya mchezo kumalizika lakini ilijikuta ikiwa nyuma kwa sheria ya mabao ya ugenini.
Nayo TP mazembe ya jamhuri ya kidemokrasi ya Congo imefikia fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika jana jumapili baada ya kutoka suluhu na wageni wao kutoka Tunisia Etoile Sahel bila kufungana katika mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali.
Na katika riadha :
Kenenisa Bekele wa Ethiopia alimpita Wilson kipsang wa Kenya aliyekuwa akishikilia rekodi ya dunia ya mbio hizo , kilomita moja kabla ya kufikia mwisho na kushinda mbio za Marathon mjini Berlin jana Jumapili. Bingwa mara tatu wa Olimpiki Bekele alishindwa hata hivyo kuifikia rekodi ya dunia kwa sekunde sita wakati akimaliza kwa kutumia saa mbili dakika 3 na sekunde 3, akiondoa dakika mbili katika rekodi yake binafsi.
Evans Chebet wa Kenya alikuwa wa tatu kwa kukimbia saa 2 dakika 05 na sekunde 31.
Nalo pambano la ngumi la marudio katika Tyson Fury na Wladimir Klitschko kwa ajili ya ubingwa wa dunia wa uzito wa juu umefutwa kwa mara ya pili. Kampuni inayofanya masuala ya kiutawala ya Fury , Hennessy Sports, imesema siku ya Ijumaa kwamba mwanamasumbwi huyo kutoka Uingereza , ameelezwa kwamba hayuko sawa kiafya kuweza kupigana na pambano la Oktoba 29 mjini Manchester , halitafanyika.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / rtre / afpe / dpae
Mhariri: Yusuf , Saumu