Schalke na FC Kolon zapata pointi mara ya kwanza msimu huu
19 Oktoba 2020Katika Bundesliga, Schalke imesogea kidogo kutoka katika nafasi ya mwisho katika msimamo wa ligi ya Ujerumani baada ya kutoka sare ya bao 1-1 jana dhidi ya Union Berlin lakini wameendeleza rekodi ya klabu hiyo kutoshinda mchezo katika michezo 20 hadi sasa. Goli la kichwa la Goncalo Paciencia liliwapa schalke pointi moja ya kwanza msimu huu wakati kocha mpya Manuel Baum akisimamia mchezo wake wa kwanza wa timu yake akiwa nyumbani. Wamesogea juu hadi nafasi ya 17, na ni Mainz 05 tu ambayo haina pointi hadi sasa imebakia katika nafasi ya mwisho, wakati FC Kolon wamesogea katika nafasi ya 16 baada ya kutoka sare na Eintracht Frankfurt jana Jumapili. Huyu hapa kocha wa Schalke 04 Manuel Baum.
"Kama mtu akiangalia mchezo huu, nafikiri hatuwezi kusema kwamba tumefurahishwa na mchezo wetu. Tumepiga hatua katika mchezo wetu , lakini mtu anatambua vipi mchezo huo umewagusa wachezaji. Na unapofungwa goli, lazima niseme wazi, kwamba nimefurahishwa, na jinsi wachezaji walivyopambana baada ya bao hilo na hatimaye kurejesha bao."
FC Kolon nao walipata pointi yao ya kwanza msimu huu, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt , ikiwa ni mwanzo mzuri kwa timu hiyo ambayo nayo imekuwa ikipata matokeo mabaya tangu mwishoni mwa msimu uliopita. Mchezaji wa FC Kolon Sebastian Bornauw alikuwa na haya ya kusema.
"Nafikiri, kwamba ni pointi muhimu kwetu. Tulikuwa na matumaini ya pointi tatu, lakini pointi moja ni bora kwa mchezo huu. Nafikiri , dakika 20 za mwanzo katika kipindi cha pili tuliweza kuonesha mchezo mzuri zaidi katika msimu huu. Ni lazima katika mchezo ujao tujaribu, kufanya kama hivi kuanzia mwanzo."
Mabingwa watetezi Bayern Munich waliikandamiza Arminia Bielefeld kwa mabao 4-1 siku ya Jumamosi baada ya Leipzig kushinda kwa mabao 2-0 nyumbani kwa Augsburg. Borussia Dortmund ilipata ushindi wa kibarua pale ilipoishinda timu inayoipa taabu sana mara kadhaa TSG Hoffenheim kwa bao 1-0 katika mchezo ambao timu zote zilionesha uwezo mkubwa. Nahodha wa Borussia Dortmund Marco Reus naye alikuwa na haya ya kusema.
"Hoffenheim imeishinda Bayern hapa wiki mbili zilizopita. Hususan jinsi walivyowashinda ilikuwa inavutia sana na leo ilikuwa tunatarajia mchezo mgumu pia. Hatujacheza mchezo mzuri sana, hii ni wazi. Lakini pia ilikuwa ni vigumu , wakati wachezaji wa timu za taifa walirejea tu siku ya Alhamis au Ijumaa. hatukuweza kufanya mazowezi ya pamoja kabisa, kwa hiyo huo ulikuwa ushindi wa kibarua. Lakini kesho hakutakuwa na mtu atakayeuliza hilo."
Timu iliyopanda daraja msimu huu VFB Stuttgart imerejea kwa kishindo katika ligi ya Bundesliga baada ya kuichapa Hertha Berlin kwa mabao 2-0 ugenini.