Schalke yajipiga kifua mbele ya Dortmund
30 Septemba 2014Mara hii mchezo huo ulimazika salama bila matukio ya kutia wasi wasi, lakini haukuisha salama kwa makamu bingwa wa ligi hiyo Borussia Dortmund , ambapo jioni hiyo walitoka vichwa chini baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya mahasimu wao hao wakubwa Schalke 04.
Borussia Dortmund ambayo imeanza msimu huu kwa kusua sua, imeonesha udhaifu mkubwa katika ulinzi ambapo hadi sasa imefungwa mabao 11 na kufunga tisa, wakiwa na pointi saba kibindoni na katika nafasi ya 12. Schalke iliyoanza msimu huu pia kwa kusua sua kwa ushindi huo imechupa hadi nafasi ya kumi ikiipita Dortmund.
Mario Goetze alikuwa nyota kwa upande wa Bayern wakati mabingwa hao watetezi wakiendelea kuwa juu ya msimamo wa ligi kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya FC Kolon licha ya kuwa kikosi cha kocha Pep Guardiola hakikung'ara kama ilivyostahili. Bayern imefikisha sasa pointi 14 kutokana na michezo sita.
Borussia Moenchengladbach ambayo iko katika nafasi ya pili iliishinda Paderborn ambayo imepanda daraja msimu huu kwa mabao 2-1, wakati Bayer leverkusen ililazimishwa sare ya bila kufungana na Freiburg.
Hamburg SV ambayo ni timu pekee ambayo haijawahi kushuka daraja nchini Ujerumani ilikuwa hadi jana Jumapili ni timu pekee ambayo haijapata bao msimu huu. Licha ya kupata bao jana dhidi ya Eintracht Frankfurt lakini kigogo hicho cha soka la Ujerumani kilishindwa kutamba na kukubali kipigo cha mabao 2-1.
Mchezaji wa kati wa Hamburg SV Tolgay Arslan alikuwa na haya ya kusema. "Tulicheza vizuri katika mchezo wote. Walikuja mara tatu katika goli letu, na wakapata bao safi kabisa. Tunaweza tu kushutumu, kwamba hatupati hata bao moja. Naamini kwamba tuliutawala mchezo huo kwa dakika 88 na hii ndio hali yetu. Tunaweza kufanya kile tunachotaka. Lakini ni lazima hali hii iendelee".
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae / rtre , ZR
Mhariri: Iddi Ssessanga