1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schalke yamfutakazi kocha wake Wagner

Sekione Kitojo
27 Septemba 2020

Klabu ya Bundesliga ya Schalke 04 imemfuta kazi  leo kocha wake mkuu David Wagner. Hatua  hiyo  imekuja  baada  ya  mwanzo wa kimaafa  katika  Bundesliga msimu  huu, ukiwa mbaya kabisa  katika  historia  ya  klabu  hiyo.

Fußball Trainer David Wagner auf Schalke entlassen
Picha: MIS/imago images

Schalke 04  inayotambulika kama  majogoo wa  bluu ya Kifalme wamekandamizwa  mabao 11 na  kufunga  bao moja  tu  katika  michezo yake  miwili  ya  mwanzo  wa  msimu  huu. Kipigo  cha  mabao 3-1 siku ya  Jumamosi nyumbani  dhidi  ya  Werder  Bremen  kimekuja  baada  ya  kipigo  cha mbwa  mwizi  cha mabao 8-0 katika  mchezo  wa  ufunguzi  dhidi  ya  mabingwa  wa  ligi Bayern Munich.

Kocha aliyetimuliwa David Wagner wa Schalke 04Picha: MIS/imago images

"Tulitarajia kwamba  tungeweza  kufanya  mabadiliko  ya  kimchezo yanayohitajika kwa pamoja  na  david Wagner," Mkuu  wa  spoti  na  mawasiliano Jochen Schneider  alinukuliwa akisema  katika  taarifa  ya  klabu  hiyo. "Kwa  bahati  mbaya  michezo yetu miwili  ya mwanzo  ya  msimu  mpya  hayakuleta mchezo unaohitajika  na  matokeo."

Makocha wasaidizi wa Wagner , Christoph Buehler  na  Frank Froehling pia wamevuliwa madraka  yao. Mrithi  wa  kazi ya  Wagner  mwenye  umri  wa  miaka  48 bado hajatangazwa. Wanaofikiriwa  kuchukua  nafasi  hiyo ni  pamoja  na  kocha  wa  zamani  wa Mainz Sandro Schwarz , kocha  wa  zamani  wa  Augsburg Manuel  Baum, kocha  wa  zamani wa  Stuttgart Alexander Zorniger na  Marc Wilmots, kocha  wa  zamani wa  Ubelgiji  ambaye pia  ni  mchezaji  wa  zamani  wa  Schalke.

Kocha wa nne kutimuliwa baada ya michezo miwili

Katika  misimu  58 ya Bundesliga, Wagner  ni  kocha  wa  nne  kuondolewa  katika  wadhifa wake  baada  ya  michezo miwili. Wengine ni Rinus Michels (FC Cologne, 1983)Morten Olsen(FC Cologne, 1995) na  Dieter Hecking (Hanover,2009).

Wachezaji wa Schalke 04 wakipeana pole baada ya kutandikwa mabao 3-1 na Werder Bremen katika BundesligaPicha: Horst Müller/Imago Images

Wagner, ambaye  alicheza  kandanda  akiwa  na  Schalke katikati  ya  miaka  ya  1990, alifungishwa  mkataba  hadi  mwaka  2022.

Wagner  aliteuliwa  kuipa mafunzo Schalke 04  majira ya  joto mwaka  jana  na  aliisaidia Schalke kufikia  nafasi  ya  tano katika  msimamo  wa  ligi katikati ya  Januari  baada  ya ushindi  wa  mabao  2-0  dhidi  ya  Borussia  Moenchengladbach kuwafikisha  pointi tatu tu nyuma  ya waliokuwa  hatimaye  mabingwa  Bayern Munich.

Lakini  Schalke  haijashinda mchezo  wa  ligi  tangu wakati  huo , na Wagner amepoteza  kazi yake  kutokana  na  hali hiyo  ya  kushindwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW