1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz aanza kusaka waziri mpya wa ulinzi

16 Januari 2023

Kansela Olaf Scholz analenga kupata waziri mpya wa Ulinzi haraka baada ya kujiuzulu Christine Lambrecht katika nafasi hiyo hii leo.

Deutschland | Verteidigungsministerin Christine Lambrecht
Picha: Sean Gallup/Getty Images

Naibu msemaji wa Kansela Scholz, Christiane Hoffmann amesema kiongozi huyo wa Ujerumani  anaheshimu maamuzi ya Lambrecht na amemshukuru kwa kazi nzuri aliyoifanya akiwa  waziri wa ulinzi.

''Kama nyote mnavyofahamu waziri wa ulinzi wa shirikisho Christine Lambrecht amemuomba Kansela amruhusu ajiuzulu.Kansela anauheshimu uwamuzi wa bibi Lambrecht na amemshukuru kwa kazi nzuri aliyoifanya katika nyakati hizi ngumu na za changamoto kama waziri wa ulinzi.Kansela atawasilisha pendekezo lake la atakayechukua nafasi hiyo kwa rais wa shirikisho katika muda mwafaka," alisema Hoffmann.

Shinikizo la kumpata waziri mpya wa ulinzi linaongezeka kutokana na ziara ya waziri wa ulinzi wa Marekani Loyd Austin anayetarajiwa kuwasili Berlin Alhamisi na atashiriki mkutano Ijumaa katika ya jeshi la Marekani mjini Ramstein kujadili suala la kuipatia msaada zaidi Ukraine.