1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz aizungumzia Ukraine katika ziara yake Afrika Kusini

24 Mei 2022

Msimamo wa Afrika Kusini katika vita vinavyoendelea vya Urusi nchini Ukraine ndio jambo kuu litakalojadiliwa wakati Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz atakapokutana kwa faragha na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa

Südafrika Besuch des Bundeskanzlers Olaf Scholz
Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Akizungumza katika mkutano na waandishi habari mjini Pretoria, kuelekea mkutano wao wa faragha viongozi wa mataifa hayo mawili ya Ujerumani na Afrika Kusini, wamesema watajadili pia suala la maendeleo ndani ya bara la Afrika. Ziara ya Scholz inafanyika wakati vita nchini Ukraine vikipamba moto kwa miezi mitatu sasa hali inayosababisha bei za bidhaa na chakula kupanda mara dufu duniani kote ikiwemo Afrika.

Afrika Kusini imechukua msimamo wa kati katika mzozo huo, ikikataa kabisa kuvikemea vitendo vya Urusi na badala yake kutoa wito wa mazungumzo kati ya mataifa hasimu.

Hata hivyo Scholz aliyekatika ziara yake ya siku tatu barani Afrika, ameeleza kuwa suala la uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ni jambo muhimu la kujadili na Rais Ramaphosa.

Kansela wa Ujerumani afanya ziara ya kwanza barani Afrika

01:24

This browser does not support the video element.

"Moja ya sualli muhimu kwetu sote linalotupa wasiwasi ni vita vilivyoanzishwa na Urusi nchini Ukraine, vita vibaya kabisa. Lazima tuseme namna hali ilivyo. Na kwa amani kutawala duniani inabidi hivi vita vimalizike haraka iwezekanavyo.

Kuna nafasi ya kutetea uadilifu na Uhuru wa Ukraine na pia kumaliza vita na kuokoa maisha ya watu wengi ambao huenda wakazidi kuangamia," alisema Scholz.

Jambo jengine muhimu litakalojadiliwa na viongozi hao wawili ni nia ya Afrika Kusini kupunguza utegemezi wake kwa mitambo ya nishati ya makaa ya mawe.

Ujerumani ni moja ya mataifa yaliyoahidi dola bilioni 8.5 kufadhili miradi ya mabadiliko ya taibia nchi katika mkutano wa COP 26 mwaka uliopita, ili kuisaidia Afrika kusini kupunguza utegemezi wa  nishati hiyo kuzalisha umeme. Lakini hadi sasa hapajakuwa na tangazo lolote la Afrika Kusini kufikia au kulipwa fedha hizo.

Ramaphosa atoa wito wa Mataifa mengine kununua chanjo za Afrika

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Picha: Phill Magakoe/AFP

Afrika Kusini inakabiliwa na mgao mkubwa wa umeme maana mitambo yake ya nishati ya mkaa wa mawe haiwezi kuzalisha umeme wa kutosha. Ramaphosa amesema fedha hizo zitaisaidia nchi yake kugeukia ulimwengu wa nishati rafiki kwa mazingira.

"Tunatarajia mijadala yenye kujenga kuhusu uchumi wa kijani,nishati safi na kujenga ustahimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi, wakati tunapoanza kufikia teknolojia mpya kama hidrojeni, na nishati nyinginezo mbadala," alisema rais Ramaphosa.

soma zaidi: Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz yupo nchini Senegal

Katika mkutano huo na waandishi habari Rais Ramaphosa pia alitoa wito kwa mataifa mengine kununua chanjo iliyotengenezwa Afrika Kusini. Aliishukuru Ujerumani kuisadia kujenga kituo cha kutengeneza chanjo hizo, lakini akasema juhudi hizo zinakabiliwa na changamoto chungu nzima kufuatia kukosa wanunuzi wa chanjo iliyotengenzwa Afrika

Scholz aliwasili Afrika Kusini baada ya kuizuru Senegal na Niger alikoelezea nia ya Ujerumani ya kupata nafasi ya uchimbaji wa gesi nchini Senegal na msaada wa kijeshi wa muda mrefu wa nchi yake kwa serikali ya Niger.

Chanzo: afp/ap

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW