1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Scholz akutana na Rais Xi siku ya mwisho ya ziara yake China

16 Aprili 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amekutana hii leo na Rais Xi Jinping mjini Beijing katika siku yake ya mwisho ya ziara ya siku tatu na kujadili masuala mbalimbali ikiwemo ushirikiano wa kiuchumi, kijiografia na kisiasa

China Peking | Rais Xi Jinping akimpokea mgeni wake Kansela wa ujerumani Olaf Scholz.
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amekutana hii leo na Rais Xi Jinping mjini Beijing katika siku yake ya mwisho ya ziara ya siku tatu na kujadili masuala mbalimbali ikiwemo ushirikiano wa kiuchumi, kijiografia na kisiasa huku pia wakigusia vita vya Ukraine, ulinzi wa hali ya hewa na mahusiano ya kibiashara baina ya nchi hizo.

Soma zaidi. Scholz na Xi kujadili juu ya China kuisaidia Urusi kijeshi

Kansela Scholz amesema ataendelea kumsisitiza Rais Xi ambaye ana uhusiano wa karibu na Rais wa Urusi,Vladmir Putin juu ya athari ya vita vya Urusi dhidi ya Ukraine kuwa vita hivyo sio tu vimeliathiri bara la Ulaya bali hata ulimwengu mzima.

Mataifa ya Magharibi yamekuwa yakiishutumu China kwamba inaipatia Urusi bidhaa ambazo zinatumika kwa madhumuni ya kiraia na kijeshi na hivyo kuipa Urusi nguvu ya kiuchumi ya kuendeleza uvamizi wake nchini Ukraine.

Scholz: Ushirikiano wetu wa kiuchumi ni muhimu

Mbali na suala hilo la Ukraine, Scholz pia ametoa mwito wa kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.

"Mheshimiwa Rais, ninafurahi kwamba tangu ziara yangu ya mwisho mnamo Novemba 2022, kumekuwa na mazungumzo ya kina na midahalo mingi kati ya serikali zetu mbili." Scholz alimwambia rais Xi.

aliongeza kuwa mashauriano ya saba kati ya serikali za Ujerumani na China yaliofanyika mjini Berlin mnamo mwezi Juni mwaka uliopita yalikuwa hatua muhimu kwa mataifa hayo ambayo ni washirika wa karibu katika masuala ya biashara.

"Siku mbili, niliongoza ujumbe wa wafanyabiashara kutembelea makampuni ya Ujerumani huko Chongqing na Shanghai. Uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi zetu mbili ni suala muhimu sana.'' amesema Kansela Scholz.

Soma zaidi. Scholz ayaweka mezani ´masuala mazito´ ziara yake China

Ujumbe wa China na Ujerumani wakiwa katika mkutano wa pamoja.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kwa upande mwingine, mwenyeji wake Rais Xi amesema wote kwa pamoja wanaweza kuimarisha utulivu na usalama duniani kama nchi hizo zikishikamana kwa kuzingatia kanuni za kuheshimiana na kutafuta suluhu licha ya tofauti baina yao.

Kuhusu masuala ya ushirikiano wa kiuchumi Xi amesema ushirikiano wa mataifa hayo ambayo yanauchumi mkubwa duniani ni muhimu katika ukuza uchumi wa Ulaya na Asia.

''Umuhimu wa kuimarisha na kuendeleza uhusiano wa China na Ujerumani unavuka upeo wa uhusiano wa pande hizo mbili na una matokeo muhimu kwa bara la Ulaya na Asia na hata dunia nzima." Rais Xi Jinping alimwambia Kansela Scholz.

Hivi karibuni, zaidi ya makampuni 5,000 ya Ujerumani ambayo yanafanya kazi nchini China yamekuwa yakilalamika kuwa yanapata hasara ikilinganishwa na makampuni ya China katika soko la kimataifa.

Mbali na hayo, Kansela Scholz anatarajiwa pia kukutana na Waziri Mkuu wa China, Li Qiang kuzungumzia mzozo unaondelea wa Taiwan ambapo zipo taarifa za kitisho kwamba China inao mpango wa kukishambulia kisiwa hicho.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW