1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz amtaka Putin kuvimaliza vita vya Ukraine

23 Novemba 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amemuhimiza Rais wa Urusi Vladmir Putin kuvimaliza vita vya Ukraine na kuwaondoa wanajeshi wake wote katika ardhi ya nchi hiyo.

Vietnam | Bundeskanzler Olaf Scholz besucht Vietnam
Kansela wa Ujerumani, Olaf ScholzPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Akizungumza Jumatano katika mkutano na waandishi habari mjini Berlin, pamoja na Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, Scholz amesema amemtolea Putin wito huo wakati wa mkutano wa kilele wa kundi la nchi zilizoendelea na zinazoinukia kiuchumi, G20, uliofanyika kwa njia ya video, ili hatimaye vita hivyo viweze kumalizika kabisa.

Putin alihudhuria kwa mara ya kwanza mkutano wa G20 tangu kuzuka kwa mzozo kati ya Urusi na Ukraine.

''Kama mnavyojua, leo rais wa Urusi ameshiriki kwa mara ya kwanza kwenye mkutano kwa njia ya video wa wakuu wa nchi na serikali wa kundi la G20, tangu alipoanzisha uvamizi dhidi ya Ukraine. Nilitoa wito kwa Rais Putin kumaliza mashambulizi yake dhidi ya Ukraine na kuyaondoa majeshi yake Ukraine ili vita hivi vimalizike kabisa,'' alifafanua Scholz.

Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni na Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Annegret Hilse/REUTERS

Scholz alisema mkutano huo wa G20, ambao aliuhudhuria pamoja na Meloni wakati wa ziara yake mjini Berlin, ulikuwa fursa nzuri kuweka wazi kuwa amani inaweza kurejeshwa kwa urahisi Ukraine kama Urusi itawaondoa wanajeshi wake nchini humo.

Scholz amesema jambo muhimu kwake ni fursa nzuri kwao kuweka wazi kwamba amani ya Ukraine iko hatarini, kwa sababu Urusi imeivamia Ukraine, na kwamba amani hiyo inaweza kurejeshwa kwa urahisi ikiwa Urusi itayaondoa majeshi yake.

Meloni apongeza ahadi ya Putin kuelekea amani

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, amesema uwepo wa Putin katika mkutano wa kilele wa G20 ulikuwa rahisi, kwa sababu hakulazimika kuondoka Moscow. Aidha, Meloni amepongeza ahadi ya Putin ya kufanya kazi kuelekea kupatikana amani ya Ukraine, lakini ameongeza kusema kuwa Urusi inapaswa kuwaondoa wanajeshi wake kwenye eneo ambalo imelivamia.

Putin hakusafiri kuhudhuria mikutano miwili ya kilele ya G20 iliyopita iliyoandaliwa na India mwezi Septemba na Indonesia mwaka uliopita, na badala yake aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov.

Rais wa Urusi Vladimir Putin, akihudhuria mkutano wa kilele wa G20Picha: Mikhail Klimentyev/AFP/Getty Images

Wakati huo huo, Rais Putin amesema kuwa Urusi haijawahi kufuta mazungumzo ya amani na Ukraine na amekataa ukosoaji unaotolewa dhidi ya uvamizi wake nchini Ukraine.

Putin pia amewalaumu viongozi wa mataifa ya Magharibi kutokana na kupanda kwa mfumuko wa bei ulimwenguni.

Putin: Urusi haijawahi kufuta mazungumzo ya amani na Ukraine

Akizungumza katika mkutano huo wa kilele wa G20, Putin amesema Urusi haijawahi kuyafuta mazungumzo ya amani kati yake na Ukraine.

Kwa mujibu wa Ikulu ya Urusi, Kremlin, Putin amesema baadhi ya washiriki wameelezea kushtushwa kwao na uvamizi wa Urusi unaoendelea katika hotuba zao. Amesema ni kweli bila shaka, vitendo vya vita wakati wote huwa ni janga, lakini Urusi haijawahi kufuta mazungumzo yoyote ya amani na Ukraine."

(DPA, AFP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW