1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz atetea uamuzi wa kuipatia Ukraine silaha

19 Mei 2022

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amelihutubia bunge la taifa na kutumia nafasi hiyo kutetea uamuzi wa serikali mjini Berlin wa kuipatia silaha Ukraine kupambana dhidi ya uvamizi wa Urusi.

Deutschland | Bundestag Regierungserklärung Olaf Scholz
Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Hotuba ya Kansela Scholz mbele ya bunge la Ujerumani, Bundestag kwa jumla ilikusanya mambo mengi lakini ilitawaliwa zaidi na suala la mzozo unaoendelea nchini Ukraine.

Scholz kwanza alitetea uamuzi wa serikali yake ya kuipatia silaha nzizo nzito Ukraine kuvikabili vikosi vya kirusi akisema hilo haliwezi kutajwa kuwa jambo linachochoea moto kwenye mzozo huo.

Kiongozi huyo amewatanabahisha wabunge na wajerumani kwamba kwa mtizamo wake kuisaidia Ukraine kwa silaha kutaiwezesha kujilinda dhidi ya mashambulizi na hiyo itakuwa njia mujarabu ya  kusitisha vita.

Matamshi yake yalikuwa yakilenga kuzitia kapuni hoja za baadhi ya watu nchini Ujerumaniambao wametoa hadhari kwamba kwa kuipatia Ukraine silaha zaidi kunautanua mzozo unaoendelea nchini humo.

Hata hivyo Scholz ametumia hotuba yake mbele ya bunge kuwakumbusha watu hao kuwa ufunguo wa kumaliza vita unapatikana Moscow. Amesema iwapo rais wa Urusi Vladimir Putin atautambua ukweli kwamba hawezi kuvishinda vikosi vya Ukraine vilivyoapa kuihami nchi yao basi vita hiyo itafikia mwisho mara moja.

Kwa tathmini ya kansela Scholz viongozi wa Kremlin  walijidanganywa pale walipopuuza utayari wa  Ukraine kujilinda dhidi ya uchokozi na rais Putin bado anadhani ataweza kulazimisha kupatikana amani nchini Ukraine kwa kutumia mabavu. Jambo hilo kansela Scholz amesema haliwezekani.

Scholz apinga Ukraine kupatiwa uanachama wa Umoja wa Ulaya haraka 

Hata hivyo mbali ya kulikingia kifua suala la Ukraine kupatiwa silaha, kansela Scholz amepinga nia ya kuikaribisha haraka Ukraine ndani ya Umoja wa Ulaya.

Amewaambia wabunge hakutakuwa na njia ya mkato kwa Ukraine kuwa mwanachama mpya wa kanda ya Ulaya licha ya uvamizi kutoka Urusi na badala yake viongozi mjini Brussels watafute njia nyingine ya kuisaidia Kyiv na siyo kupitia turufu ya ahadi ya uanachama.

"Ukweli kwamba hakuna njia ya mkato ya kuingia ndani ya Umoja wa Ulaya ni suala linalohusu kuyatendea haki pia mataifa sita ya Balkani magharibi. Kwa miaka mingi yamekuwa yakifanya mageuzi makubwa na kujitayarisha kwa uanachama" amesema Scholz.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine Dmytro Kuleba Picha: Olivier Matthys/AP Photo/picture alliance

Kwenye hoja hiyo Scholz alikuwa akiyatetea mataifa sita ya Montenegro, Serbia, Albania, Macedonia Kaskazini ,Bosnia/Herzegovina na Kosovo yaliyoomba siku nyingi kuwa wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Hata hivyo msimamo huo wa Scholz ambao unafanana na ule uliotolewa na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, yumkini hautawafurahisha viongozi wa Ukraine.

Na muda mfupi tu baada ya hotuba ya kansela Scholz waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine Dmytro Kuleba ameukosoa vikali msimamo wa baadhi ya viongozi wa Ulaya akisema baadhi ya matiafa ya ulaya yanaizingatia nchi yake kuwa ya tabaka la pili.

Lakini mbali ya Scholz kupinga uanachama wa wa haraka wa Ukraine ndani ya umoja wa ulaya,ametangaza kuunga mkono msaada wowote wa ziada utakaohitajika kuisaidia nchi hiyo wakati wa vita na hata baada.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW