1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz aunga mkono mpango wa kuwarudisha makwao wahalifu

6 Juni 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameunga mkono mpango tata wa kuwarudisha makwao wahalifu raia wa Afghanistan na Syria wanaoishi Ujerumani.

Berlin | Olaf Scholz - Bunge la Ujerumani
Kansela wa Ujermani Olaf Scholz akilihutubia bunge la Ujerumani BundestagPicha: Political-Moments/IMGAO

Akilihutubia bunge la Ujerumani Bundestag mapema leo, kiongozi huyo amesema wahalifu sugu hawana nafasi ndani ya Ujerumani licha ya kupewa hifadhi nchini humo. 

Akilihutubia bunge mapema leo, Kansela Olaf Scholz amejikita katika masuala matatu muhimu: mpango wa kuwarudisha makwao wahamiaji wahalifu katika nchi ambazo zinatajwa kuwa sio salama, mafuriko yaliyoikumba Ujerumani hivi karibuni na uungwaji mkono wa Ujerumani kwa Ukraine.

Scholz amesema masuala hayo matatu hayana uhusiano wa moja kwa moja, ila yanawahusu.

Soma pia: Maelfu wahamishwa kusini mwa Ujerumani kufuatia mafuriko 

Alianza hotuba yake kwa kuangazia kifo cha afisa wa polisi aliyeuawa kwa kudungwa kisu na raia wa Afghanistan mwenye umri wa miaka 25 wiki iliyopita. Scholz ameeleza kuwa tukio hilo limegusa mioyo ya Wajerumani wote.

Kiongozi huyo amelaani kile alichokiita "misimamo ya kidini yenye itikadi kali” ambayo inatishia kuwanyang'anya uhuru wao.

Wahalifu na vitisho vya kigaidi havina nafasi hapa. Hali hiyo inapotokea, maslahi ya usalama ya Ujerumani ni muhimu kuliko maslahi ya wahalifu.

Wabunge wakisikiliza hotuba ya Kansela Olaf Scholz mjini BerlinPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Akizungumza na familia, marafiki na wafanyikazi wa polisi aliyeuawa, Scholz amesema anasimama nao kwa dhati. Amesisitiza haja ya kuwekwa sheria kali dhidi ya matukio kama hayo ya uhalifu na kwamba wote wanaowaua polisi wanapaswa kuadhibiwa vikali.

Kuhusu mpango tata wa kuwarudisha makwao wahamiaji wahalifu, ameonyesha kuchukizwa na tabia ya watu waliopewa hifadhi nchini Ujerumani kujihusisha na uhalifu.

Soma pia:  Macron na Scholz wazungumzia mzozo wa Ukraine

Scholz amesema watu kama hao wanapaswa kufurushwa Ujerumani na kurudishwa makwao. Suala la iwapo Ujerumani inapaswa kuanza tena kuwarudisha makwao wahalifu raia wa Afghanistan na Syria, limezua mjadala mpana nchini humo.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha kikosi cha polisi na kuahidi kuwa Ujerumani itawanyima uraia watu wenye mafungamano na makundi ya itikadi kali za dini au wenye misimamo ya chuki dhidi ya Wayahudi na kwamba mamlaka haitofikiria mara mbili kuwatimua watu wenye sifa hizo.

Scholz: Mafuriko ni janga linalohitaji kushughulikiwa

Athari ya mafuriko yaliyoikumba jimbo la BavariaPicha: Michael Bihlmayer/Bihlmayerfotografie/IMAGO

Ama kuhusu mafuriko yaliyokumba eneo la kusini mwa Ujerumani mwishoni mwa wiki, Scholz ametoa risala za rambirambi kwa waathiriwa na kuwashukuru wote waliotoa mkono wa usaidizi.

Kansela huyo ameeleza kuwa, juhudi za mtu mmoja mmoja, serikali za mitaa, majimbo na serikali kuu ni ishara kwamba "Umoja ni nguvu.”

Amesema mafuriko hayo ya mwisho mwa wiki ni ya tatu kuikumba Ujerumani tangu mwanzoni mwa mwaka huu huku akilitaja janga hilo kama ishara ya wazi ya muendelezo wa taathira ya mabadiliko ya tabianchi.

Soma pia: Scholz: Muda wa Ujerumani kuwa na rais mwanamke umefika 

Ama kuhusu vita nchini Ukraine, kiongozi huyo wa Ujerumani kwa mara nyengine amesisitiza kuiunga mkono Kyiv na kueleza kuwa kupatikana kwa amani sio tafsiri ya kujisalimisha au kukubali kushindwa.

"Urusi imeanza mashambulizi mapya katika wiki za hivi karibuni. Kharkiv, mji wenye mamilioni ya watu ulio mpakani na Urusi unashambuliwa na makombora ya Urusi  karibu kila siku. Nyumba, maduka, shule na viwanda vimelengwa, kama hiyo haitoshi, rais wasiokuwa na hatia, wanawake, wanaume na watoto pia wanashambuliwa.”

Akizungumzia juu ya kinachoendelea katika uwanja wa vita nchini Ukraine, Scholz amekosoa wabunge wa AfD kwa kukatiza hotuba yake mara kwa mara.

Amekemea tabia hiyo na kusema inatia aibu kwa AfD kupokea sifa kutoka kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye ameweka wazi kuwa hana tatizo lolote kushirikiana na chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia.

Jana Jumatano, Putin alisema yuko tayari kushirikiana na wote wanaotaka usuhuba na Urusi kikiwemo chama cha AfD ambacho kimekumbwa na msururu wa kashfa zinazohusisha wagombea wake wakuu katika uchaguzi wa bunge la Ulaya wiki hii na Kremlin.

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi