1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz autaja uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kuwa ubeberu

Josephat Charo
21 Septemba 2022

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amekosoa vikali uvamizi wa Urusi nchini Ukraine akiuita ubeberu na kutoa wito wa ushirikiano zaidi ili kudumisha utaratibu wa mfumo wa dunia wa utawala.

UN Generalversammlung | Olaf Scholz
Picha: Eduardo Munoz/REUTERS

Akizungumza katika kikao cha jana cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameuitaja uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kama kitendo cha ubeberu. Scholz aliikosoa vikali Urusi kwa kuivamia Ukraine, akilalamika juu ya msukumo na motisha wa rais Vladimir Putin kuhusiana na vita hivyo. Amesema hakuna uhalali wowote wa vita vya Urusi kuivamia Ukraine na Putin anaendesha vita kwa lengo moja tu la kutaka kuiteka Ukraine.

Scholz ametoa mwito kwa nchi wanachama zisiegemee upande wowote katika vita hivyo huku akigusia suala la silaha za nyuklia inazomiliki Urusi. Kansela huyo wa Ujerumani amesisitiza juu ya umuhimu wa kuendeleza na kuulinda mfumo wa dunia wa kiutawala uliojikita katika msingi wa sheria.

"Kurejea kwa ubeberu sio tu janga kwa Ulaya bali pia kwa mfumo wetu wa kimataifa wa amani, ambao ni kinyume cha ubeberu na ukoloni mamboleo. Pamoja na washirika wetu duniani kote, tumeuwekea vikwazo vikali vya kiuchumi uongozi na uchumi wa Urusi. Na hivi ndivyo tunavyotimiza ahadi ambayo kila nchi ilitoa wakati wa kujiunga na Umoja wa Mataifa; kuunganisha nguvu ili kudumisha amani na usalama wa kimataifa."

Macron ahutubia kwa mara ya kwanza

Akizungumza kwa mara ya kwanza katika mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema mazungumzo ya kuutanzua mgogoro wa vita yatafanikiwa tu ikiwa uhuru wa Ukraine utaheshimiwa, maeneo yake kukombolewa na usalama wake kulindwa.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, kulia, akiwa na waziri Mkuu wa Uingereza, Liz Truus jijini New YorkPicha: Stefan Rousseau/AP/picture alliance

Macron pia alisema Urusi inatakiwa kufahamu kwamba haiwezi kulazimisha inachokitaka kutumia nguvu za kijeshi hata kama itaziunganisha na kura za maoni katika maeneo yaliyoshambuliwa kwa mabomu na ambayo sasa inayakalia. "Ni jukumu la wanachama wa baraza la usalama kusema kwa sauti kubwa na ya wazi na kwa wanachama wa baraza hili kutusaidia katika njia hii ya kuelekea amani. Nawatolea wito wanachama wa Umoja wa Mataifa wachukue hatua ili Urusi iachane na chaguo la vita, ipime gharama ya vita kwake na kwetu sote na ikomeshe uchokozi wake"

Macron aidha alisema Ufaransa itafadhili usafirishaji wa ngano ya Ukraine kwenda Somalia, nchi inayokabiliwa na kitisho cha njaa.

Waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez alimkosoa rais wa Urusi Vladimir Putin kwa kuivamia Ukraine akisema hakuna amani kukiwa na njaa na haiwezekani kukabiliana na njaa bila amani.

Kwa upande wake Mfalme Abdullah wa pili wa Jordan alisema kwa watu wengi duniani ukweli unaoendelea kukua ni kuhusu baa la njaa. Alisisitiza kuwa nchi zinazoendelea ndizo zilizoathiriwa zaidi na kuhoji ikiwa huu ndio mustakabali tunaotaka kuviachia vizazi vijavyo.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, rais wa Senegal Macky Sall alisema tangu mkutano wa mwisho wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa, dunia imegeuka kuwa hatari zaidi na kutotabirika huku ikikabiliwa na athari za ongezeko la joto, changamoto za kiusalama na vita nchini Ukraine.

Rais wa Marekani Joe Biden atauhutubia mkutano huo hivi leo ambapo anatarajiwa kutangaza msaada mpya kwa Ukraine.

(afpe)