Scholz awahimiza wakulima Ujerumani kabla ya mgomo mkubwa
13 Januari 2024Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ametoa wito wa kuwepo utulivu na utayari wa kukubali maafikiano wakati nchi ikikabiliwa na maandamano ya wakulima wenye hasira kuhusu mpango wa kupunguza ruzuku yao ya mafuta. Scholz ameonya kuhusu watu wenye itikadi kali wanaochochea hasira miongoni mwa umma.
Soma pia:Scholz kukutana na wawakilishi wa wakulima Alhamis
Wakulima walifunga barabara kuu na kuvuruga usafiri kote nchini kwa kutumia matrekta yao kama sehemu ya wiki ya maandamano ya kupinga mpango wa kuondoa ukomo wa kodi ya dizeli inayotumika katika kilimo. Kansela Scholz amesema leo katika ujumbe wa video kuwa serikali ilizichukua kwa umakini hoja za wakulima na kusisitiza kuwa serikali ilifikia maelewano mazuri, ijapokuwa wakulima wanaendelea kusisitiza kuhusu kubatilishwa kikamilifu kwa mpango wa kupunguzwa kwa ruzuku. Aidha amesema kuwa maafisa watajadili nini kingine wanaweza kukifanya ili sekta ya kilimo iwe na mustakabali mwema.