1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Scholz na Biden wahimiza kuidhinishwa msaada kwa Ukraine

10 Februari 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Rais Joe Biden wa Marekani wamelitolea wito bunge la Marekani kuidhinisha msaada uliocheleweshwa wa kijeshi kwa ajili ya Ukraine, na kuonya Kyiv haiwezi kufanikiwa bila ya msaada huo.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz nchini Marekani
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz (kushoto) alipokutana na Rais Joe Biden wa Marekani kujadiliana namna wanavyoweza kuongeza shinikizo kwa bunge la Marekani kuruhusu msaada wa kifedha kwa Ukraine Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kansela Scholz ambaye nchi yake ni muungaji mkono mkubwa wa kijeshi wa Ukraine, ikifuatiwa na Marekani amesema anatumai kutafikiwa makubaliano ya kuidhinisha msaada huo wa mabilioni ya dola. Wakuu hao wamezungumza hayo katika ofisi ya Rais Joe Biden, mjini Washington.

Scholz ameonya kwamba bila ya msaada wa Marekani na kuungwa mkono na mataifa ya Ulaya, ni dhahiri kwamba Ukraine isingeweza kuitetea nchi yake.

Mapema, Scholz aliwaambia waandishi wa habari kwamba ametiwa moyo na hatua ya Baraza la Seneti la Marekani siku ya Alhamisi kukubali kuanza kuuangazia mpango utakaoidhinisha msaada wa kijeshi wa dola bilioni 60 kwa Ukraine.

Soma pia:Mkutano wa Scholz na Biden, kipi kitarajiwe?

Hata hivyo, mashaka yamesalia ikiwa wahafidhina wenye msimamo mkali katika Baraza la Wawakilishi litapitisha muswada huo.

Haiko wazi ikiwa Baraza la Wawakilishi nchini Marekani litaidhinisha msaada wa kifedha kwa ajili ya Ukrane ambayo inapambana na UrusiPicha: Leigh Vogel/Getty Images for Resist Trumpism

Mkwamo wa kisiasa waisababishia Kyiv kupungukiwa silaha

Mkwamo kisiasa mjini Washington umesababisha Kyiv kupungukiwa silaha, katika wakati ambapo wanajeshi wa Urusi wakisonga mbele taratibu katika mashambulizi ya majira ya baridi huko mashariki mwa Ukraine.

Soma pia:Scholz: Ninataraji kuwa Bunge la Marekani litaafikiana kuhusu msaada kwa Ukraine

Baraza la Seneti la Marekani linajadili muswada wa kuanza tena kuepeka silaha kulisaidia jeshi la Ukraine lililoelemewa, ingawa hata kama utapitishwa bado utakabiliwa na kizingiti kigumu zaidi katika Baraza la Wawakilishi linaloongozwa na wabunge wa Republican.

Wabunge hawa wanajaribu kuzuia misaada kwa Ukraine, wakishinikiza hatua kali zaidi kuchukuliwa katika kudhibiti uhamiaji haramu katika mpaka wa Mexico.

Wiki iliyopita viongozi wa Umoja wa Ulaya hatimaye walifanikiwa kuukabili mkwamo uliosababishwa na kiongozi wa mrengo wa kulia wa Hungary Viktor Orban na kuidhinisha yuro bilioni 50 za msaada wa kiuchumi kwa Ukraine.

Rais wa Urusi Vladimir Putin (kulia) alipozungumza na mtangazaji wa Marekani Tucker Carlson hivi karibuniPicha: Tucker Carlson Network/Zuma Press Wire/dpa/picture alliance

Putin ni "muongo"

Scholz aidha, alimshutumu Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa kile alichosema "uwongo mkubwa" katika mahojiano na mtangazaji wa Marekani, Tucker Carlson yaliyorushwa jana Alhamisi.  "Anataka kupata maeneo ya majirani zake. Ni ubeberu tu," alisema.

Biden hata hivyo, hakujibu alipoulizwa ikiwa watalizungumzia suala la mwandishi wa Jarida la Wall Street la Marekani, Evan Gershkovich, aliyefungwa gerezani nchini Urusi.

Putin alidokeza kwenye mahojiano hayo kwamba alikuwa na nia ya kubadilishana wafungwa ambapo mwandishi huyo wa habari wa Marekani angeachiliwa kama sehemu ya makubaliano ambayo Ujerumani itamwachilia huru raia wa Urusi aliyepatikana na hatia ya kumuua muasi wa zamani wa Chechnya aliyetoroka huko mjini Berlin.

Kwenye mkutano huo, Scholz na Biden wamegusia pia juu ya kuongezeka kwa mvutano huko Mashariki ya Kati, wakati vita vya Israel dhidi ya Hamas vikiwa havionyeshi dalili ya kupungua na kwa upande wingine, Washington ikiwa imeanzisha mashambulizi dhidi ya maeneo yanayohusishwa na Iran kufuatia mashambulizi dhidi ya wanajeshi wake.