Scholz: Elon Musk anatishia demokrasia ya Ulaya
17 Januari 2025Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema kwamba bilionea wa teknolojia wa nchini Marekani Elon Musk anatishia demokrasia ya Ulaya kutokana na mashambulizi yake dhidi ya viongozi wa kisiasa na kuunga mkono mrengo wa kulia.
Kansela Scholz ameongeza kuwa "Musk anauunga mkono mrengo wa kulia kila mahali hapa Ulaya. Uingereza, Ujerumani na mataifa mengine mengi. Na hicho ni kitu kisichokubalika kabisa. Kinahatarisha maendeleo ya demokrasia, Ulaya. Kinaiharibu jamii yetu. Na hilo linatakiwa kupingwa. Anasimama na mrengo wa kulia, iwe kwa maslahi ya kibiashara ama kwa sababu zitakazoegemea msimamo wake wa kisiasa, hilo halikubaliki."
Musk, mtu tajiri zaidi duniani, ameibua ghadhabu kote barani Ulaya kwa msururu wa mashambulizi dhidi ya viongozi wa bara hilo, akiwemo Scholz na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer.
Soma: Scholz, Habeck waelezea wasiwasi kuhusu Musk na AfD
Idadi kubwa ya wabunge wa Bunge la Ulaya wiki hii walielezea "wasiwasi mkubwa" juu ya uingiliaji wa Musk katika siasa za Ulaya, kwenye barua kwa Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen.
Mapema mwezi huu Musk, alimkaribisha Alice Weidel, mgombea wa Ukansela wa Ujerumani kwa chama cha AfD, katika mahojiano ya moja kwa moja kwenye jukwaa lake la mtandao wa kijamii wa X.
Scholz alisema si kwamba anakosoa ukweli kwamba "bilionea kutoka nchi nyingine anazungumza mawazo yake katika ulimwengu wa kimataifa".