Scholz, Habeck waelezea wasiwasi kuhusu Musk na AfD
4 Januari 2025Scholz, wa chama cha Social Democratic (SPD), ameliambia jarida la Stern katika makala iliyochapishwa Jumamosi, kwamba ingawa hajashtushwa na kauli za Musk dhidi yake na wanasiasa wengine wa Ujerumani, uungwaji mkono wa Musk kwa chama hicho cha mrengo wa kulia unatia wasiwasi zaidi.
Shirika la kijasusi la ndani la Ujerumani la BfV linakifuatilia chama cha kitaifa cha AfD kama kikundi kinachoshukiwa kuwa na itikadi kali za mrengo wa kulia, na mashirika kadhaa ya ngazi ya majimbo tayari yamekiorodhesha kuwa cha mrengo huo.
Habeck, mgombea wa chama cha Kijani katika uchaguzi ujao, amemuonya Musk, ambaye ni mfuasi mkubwa wa Rais mteule wa Marekani Donald Trump, dhidi ya kuingilia uchaguzi wa Ujerumani. Habeck amesema katika jarida la habari la Spiegel kuwa "Mchanganyiko wa utajiri mkubwa, udhibiti wa habari na mitandao ya kijamii, matumizi ya akili mnemba (AI) na nia ya kupuuza sheria ni shambulio la moja kwa moja kwa demokrasia ya Wajerumani."