1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz na upinzani walumbana bungeni kuhusu uhamiaji

11 Septemba 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na upande wa upinzani wamekabiliana bungeni baada ya pande hizo mbili kushindwa kukubaliana kwenye mazungumzo kuhusu uhamiaji.

Kansela wa Ujerumani bungeni
Kansela wa Ujerumani bungeniPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kansela Scholz ametetea sera ya serikali yake ya uhamiaji. Alisisitiza hilo alipohutubia bungeni leo Jumatano pamoja na haja ya nchi ya Ujerumani ya kuwavutia raia wa kigeni wenye ujuzi.

Kufuatia kushindikana kwa mazungumzo ya uhamiaji kati ya serikali na upande wa upinzani, Kansela Scholz wa chama cha SPD na upinzani wa vyama vya CDU na CSU wameelekezeana shutuma nzito bungeni.

Katika mjadala wa jumla wa wiki ya bajeti, Kansela Scholz amevilaumu vyama vya CDU na CSU kwa kushinikiza kauli mbiu na kufanya maigizo katika sera ya uhamiaji. Wakati huo huo, hata hivyo, amejitolea kuendelea na mazungumzo baada ya yote hayo kutokea. Scholz amesema mlango wa mazungumzo ya uhamiaji kati ya serikali yake na upinzani, haujafungwa na kwamba wataendelea kufanya mazungumzo na upinzani iwapo wataridhia.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha CDU Friedrich Merz bungeni. Picha: Ebrahim Noroozi/AP/picture alliance

Lakini kiongozi wa chama cha upinzani cha kihafidhina cha Christian Democratic Union, CDU Friedrich Merz, amelikataa pendekezo hilo la kuendelea na mazungumzo, amesema mapendekezo ya serikali juu ya kukabiliana na uhamiaji usio wa kawaida yana mapungufu na pia hayakidhi haja.

Kansela wa Ujerumani alimjibu kiongozi huyo wa upinzani mbele ya wabunge kwamba uongozi sio sawa na kupanda vilima kwa kutoa madai na kujifanya mwamba bali uongozi ni kujua na kuwa na uwezo wa kuwashawishi watu wako na kufikia makubaliano.

Soma Zaidi: Ujerumani kuongeza kasi ya kuwarudisha wahamiaji makwao 

Wakati idadi ya wahamiaji kuja barani Ulaya ikiendelea kupanda katika kipindi cha karibu muongo mmoja, hali hiyo inachochea upinzani na ukuaji wa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia.

Baadhi ya watu wanaolalamika wanasema huduma za kijamii zimezidiwa nguvu, na mashambulizi ya watu wenye itikadi kali wanaotafuta hifadhi nchini Ujerumani yanazidisha hofu ya usalama nchini humu.

Chanzo: DPA

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi