1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz: Tunahitaji kuishirikisha Urusi kusaka amani Ukraine

9 Septemba 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema anaamini wakati umefika wa kuishirikisha Urusi kwenye mazungumzo ya kutafuta amani katika vita vyake na Ukraine.

Kansela Olaf Scholz na rais Zelensky
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz (kulia) na rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine (kushoto)Picha: Boris Roessler/Pool via AP/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akizungumza na kituo kimoja cha habari nchini aliweka wazi kwamba anaamini wakati umefika wa kuikaribisha Urusi kwenye mazungumzo ya kumaliza vita Ukraine.

Scholz alisema yeye pamoja na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine wamekubaliana kwamba Urusi inapaswa kushirikishwa katika mazungumzo yajayo ya kutafuta amani yenye lengo la kumaliza vita hivyo vinavyoendelea.Soma pia: Kremlin: Urusi itashambulia Ulaya iwapo Marekani itapeleka makombora Ujerumani

"Naamini hivi sasa muda umefika wa kujadili namna tutakavyojiondowa kwenye hali hii ya vita na kufikia amani haraka iwezekanavyo na kuimaliza hali hii ya sasa. Bila shaka utakuwepo mkutano mwingine wa amani na rais wa Ukraine pamoja na mimi tumeshakubaliana kwamba tunapaswa kuijumuisha Urusi.''

Upinzani wamkosoa Kansela Scholz

Hata hivyo, msimamo wa kiongozi huyo wa Ujerumani umekosolewa vikali na chama cha upinzani cha wahafidhina cha Christian Democtratic Union, CDU huku msemaji wa sera za nje wa chama hicho Roderich Kiesewetter akisema kiongozi huyo ameshanasa kwenye mtego wa propaganda za Urusi.

Mwanasiasa wa CDU Roderich Kiesewetter akiwa bungeniPicha: Jean MW/Future Image/IMAGO

Amesema mabadiliko hayo ya msimamo wa Kansela Scholz yanakejeli azimio maarufu lililotolewa dhidi ya Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo mwaka 2022,lililoifanya Ujerumani kubadili sera zake za kiusalama.

Amekwenda mbali zaidi msemaji huyo wa CDU wa masuala ya sera za nje, kwa kusema Kansela Scholz anajaribu kujinadi kama kiongozi mpenda amani, lakini kwa gharama ya Ujerumani na washirika wake na hilo linazidisha hali kubwa mbaya nchini Ukraine na pia kuudhoofisha Umoja wa Ulaya na usalama wa Ujerumani. Soma pia: Ujerumani yasema bajeti finyu haitawazuia kuisaidia Ukraine

Msimamo huu mpya wa Kansela wa Ujerumani kuhusu suala la mazungumzo na Urusi umetolewa katika kiwingu cha madai ya kutokea mashambulizi ya droni za Urusi,dhidi ya mataifa mawili wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO ambayo ni jirani na Ukraine.

Imeripotiwa kwamba droni za Urusi ziliangukia kwenye ardhi ya Romania wakati nchi hiyo ikiishambulia Ukraine usiku huku  droni nyingine ikiangukia Mashariki mwa Latvia.

Ndege ya kivita aina ya Falcon ikiondoka kambi ya kijeshi ya Spangdahlem UjerumaniPicha: U.S. Air Force/ZUMA/picture alliance

Nchi zote mbili washirika wa Ukraine, Jumapili zilitangaza kuanzisha uchunguzi wa matukio hayo. Matukio hayo pia yameibuwa miito ya maafisa kadhaa ya kutaka hatua zichukuliwe kwa pamoja kukabiliana na mashambulio ya anga ya Urusi.

Naibu katibu mkuu wa jumuiya ya NATO Mircea Geoana amelaani matukio hayo akiyaita ya kutowajibika na yanayoweza kusababisha hatari lakini pia akibaini kwamba hakuna ishara zinazoonesha yalifanyika kwa makusudi kuyalenga mataifa wanachama wa muungano huo wa kijeshi.

Soma pia: Vyama rafiki na Urusi Ujerumani vyapata mafanikio

Wakati hayo yakiendelea mwanadiplomasia wa ngazi za juu wa Chin Wang Yi anajiandaa kuitembelea Urusi wiki hii atakakoshiriki mkutano kuhusu usalama utakaoyakutanisha mataifa wanachama wa kundi la BRICS.

Mkutano huo utafanyika Jumatano hadi Alhamisi huko St. Petersburg na utawaleta pamoja maafisa wa ngazi za juu wanaohusika na usalama pamoja na washauri wa masuala ya usalama wa mataifa yao.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW