1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

Scholz afurahi Brazil kurejea katika jukwaa la kimataifa

31 Januari 2023

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amesema amefurahi kuona kuwa Brazil imerejea katika jukwaa la kimataifa na anatazamia kuwepo ukurasa mpya wa uhusiano na Brazil.

Brasilien | Olaf Scholz in Brasilia
Picha: Ueslei Marcelino/REUTERS

Scholz ameyatoa matamshi hayo Jumatatu mjini Brasilia, baada ya kukutana na Rais Luiz Inacio Lula da Silva ambaye aliapishwa Januari Mosi, kufutia kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Jair Bolsonaro kuondoka madarakani katika hali yenye utata.

Scholz ambaye yuko kwenye kituo cha mwisho cha ziara yake ya siku nne katika nchi za Amerika Kusinibaada ya kuizuru Chile na Argentina, amemuhakikishia Lula uungaji mkono wake kutokana na uvamizi wa majengo ya serikali yaliyofanywa na wafuasi wa Bolsonaro waliokuwa wakipinga ushindi wa urais wa Lula. 

Kuna umuhimu wa kutetea demokrasia

''Nimefurahi kuwa hapa leo, kwa sababu picha za uvamizi wa bunge, Ikulu ya Planalto na Mahakama ya Juu ya Shirikisho wiki tatu zilizopita, bado zinatupa kumbukumbu ya masikitiko makubwa. Bado tunashuhudia jinsi majengo haya yalivyoharibiwa. Uvamizi huo kwa kweli ni ishara kwetu kutetea demokrasia,'' alifafanua Scholz.

Scholz amesema lazima wasimame pamoja kwa lengo la kutetea demokrasia na wanafurahi kuona Brazil imejitolea kwa ushirikiano mkubwa wa kikanda katika nchi za Amerika Kusini. Amesema baada ya kumkosa Lula, sasa wote wana mipango mikubwa na wanatazamia ushirikiano mzuri wa muda mrefu.

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz akiwa na Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da SilvaPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Aidha, Scholz ameahidi kuipatia Brazil euro milioni 200 kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo katika nishati ya kijani na kuutunza msitu wa Amazon kwa kuanzisha miradi ya kupanda miti. Kansela huyo wa Ujerumani amesema Brazil ina jukumu kubwa na muhimu katika kuusaidia ulimwengu katika kipindi cha mpito kuelekea katika matumizi ya nishati safi na kuimarisha ulinzi wa mazingira. Kwa upande wake Lula ameahidi kupambana na mabadiliko ya tabianchi na anataka kupunguza kasi ya ukataji miti katika msitu wa Amazon.

Kuhusu vita vya Ukraine, Scholz amesema Ujerumani na Brazil zote zina msimamo sawa, huku serikali za nchi hizo zikilaani vikali uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Brazil kutopeleka mitambo ya kurushia mizinga 

Hata hivyo, Lula amesema nchi yake haitoipeleka mitambo ya kurushia mizinga kwa ajili ya vifaru chapa Leopard, ambavyo Ujerumani imeahidi kuipatia Ukraine. Brazil pia haitotoa mitambo hiyo kwenye vifaru chapa Gepard kwa ajili ya mfumo wa ulinzi wa anga ambavyo tayari Ujerumani imeipatia Ukraine.

''Brazil ni nchi ya amani, na hivyo hatutaki kujiingiza katika vita hivi, hata kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kwa sababu nadhani kwa wakati huu dunia inapaswa kuangalia wale ambao wanaweza kusaidia kutafuta amani kati ya Urusi na Ukraine,'' alisisitiza Lula. Kiongozi huyo wa Brazil amesema neno ''amani'' linatumika kidogo sana. Aidha, Scholz amesema Urusi inapaswa kuwaondoa wanajeshi wake Ukraine ili mazungumzo ya amani yaweze kufanyika.

Katika hatua nyingine Kansela huyo wa Ujerumani ametangaza kuanzisha tena majadiliano kati ya serikali za Ujerumani na Brazil, yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2015. Majadiliano hayo yalisitishwa wakati wa utawala wa Bolsonaro.

(DPA, AFP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW