1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz: Nitahimiza mkakati mpya kuelekea Ulaya Mashariki

Sylvia Mwehozi
12 Agosti 2021

Waziri wa fedha wa Ujerumani na mgombea wa ukansela kwa tiketi ya chama cha Social Democrats SPD, Olaf Scholz amesema akiingia madarakani atahimiza sera mpya juu ya Urusi na nchi nyingine za Ulaya mashariki.

DW Interview BTW Olaf Scholz SPD
Picha: Ronka Oberhammer/DW

Scholz ameyasema hayo katika mahojiano maalum na DW, na kusema kwamba kuna haja ya kurejea katika "misingi ya pande zote" kwa ajili ya usalama na haki za binadamu barani Ulaya iliyokubaliwa chini ya shirika la usalama na ushirikiano wa kiuchumi  barani humo OSCE, linalowezesha mdahalo kati ya nchi za magharibi na mashariki.

Bwana Scholz ameeleza kwamba Urusi na nchi nyingine zinapaswa kukubali kwamba ushirikiano wa Ulaya utaendelea na kama kunahitajika kudumisha usalama wa pamoja, basi Umoja wa Ulaya lazima uwasiliane na Urusi.

Hata hivyo mgombea huyo wa SPD amesema hatua ya Urusi ya kuliteka jimbo la Crimea ni tatizo kubwa linaloendelea kuchochea mivutano mashariki mwa Ukraine. "Ndio maana ni lazima kwamba turejee kwenye utawala wa sheria. Mabavu hayafanyi mambo kuwa sawa", alisema Scholz akiongeza kuwa.

"Tunachohitaji ni mkakati mpya kuelekea Ulaya mashariki ambao utaimarisha wazo hili la OSCE. Hatutaki kurudi kwenye siasa za karne ya 17,18 na 19 ambako mataifa yaliyo na nguvu hufanya siasa wenyewe. Ni juu ya Umoja wa Ulaya na Urusi kama tunataka kuwa na usalama wa pamoja wa Ulaya".

Kauli yake inatolewa katikati mwa mvutano unaozidi kuongezeka baina ya Umoja wa Ulaya na Belarus juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu na katikati mwa mvutano unaoendelea na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya Poland na Hungary juu ya kile Brussels inachokielezea kama ukiukaji wa utawala wa sheria.

Mgombea huyo pia aligusia janga la Covid-19 akisema Ujerumani inalo jukumu la kuhakikisha kuwa chanjo za kutosha zinazalishwa kwa ajili ya nchi zenye mahitaji.

Kama waziri wa fedha wa Ujerumani wakati wa janga hili la Covid-19, Scholz alisimamia uidhinishwaji wa fedha za kuokoa uchumi wa euro bilioni 400 lakini ametupilia mbali ukosoaji kwamba fedha hizo hazitoshi kushughulikia pengo la ukosefu wa kiuchumi linalozidi kuongezeka kutokana na janga hilo.

Suala la wakimbizi, nalo liliibuka katika mahojiano ya Scholz na DW, hasa wakati huu ambapo idadi kubwa ya raia wa Afghanistan wanayakimbia mapigano, suala hilo bila shaka litazua mjadala katika uchaguzi mkuu wa Septemba. Alipoulizwa ni vipi atashughulikia uwezekano wa wimbi jipya la wakimbizi wanaowasili, Scholz amesema kipaumbele hivi sasa wanapaswa kugeukia utoaji wa misaada kwenye nchi ambako wakimbizi huwasili kwa mara ya kwanza badala ya kutoa ahadi ya kuwapokea wakimbizi zaidi hapa Ujerumani.

Katika wiki za hivi karibuni, SPD imekuwa ikijikokota kati ya asilimia 15 na 18 nyuma ya muungano wa kihafidhina wa Kansela Angela Merkel wa CDU/CSU unaoongozwa na Armin Laschet. Lakini kura za maoni za hivi karibuni zinaashiria kuwa chama cha SPD cha Scholz kinaweza kuunda serikali kwa kushirikiana na chama cha kijani na kile cha mrengo wa kushoto Die Linke.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW