1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUbelgiji

Scholz: Uamuzi wa EU unapaswa kuwa ishara pia kwa Putin

14 Desemba 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema makubaliano ya pamoja yatakayoifaa Ukraine katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussles, yatakuwa ishara muhimu sana kwa Kiev na vilevile kwa Moscow.

Belgien Brüssel | EU-Gipfel | Bundeskanzler Olaf Scholz
Picha: Hatim Kaghat/dpa/picture alliance

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Brussels Ubelgiji, wanahitaji uamuzi wa pamoja, ikiwa wataanzisha mazungumzo ya uanachama na Ukraine na vilevile kuidhinisha mpango wa muda mrefu wa kuipa msaada wa kifedha wa takriban euro bilioni 50. Maamuzi ambayo mara kwa mara, waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban ametishia kuyapinga.

Katika tukio jingine, mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg ametahadharisha kuwa kuna kitisho halisi kwamba Rais Putin hatakoma na Ukraine ikiwa atapata ushindi wa kijeshi huko. Amesisitiza kuwa kitisho hicho ni sababu tosha kwa washirika wa NATO na Ukraine kuendelea kuiunga mkono kijeshi Kyiv.

Kulingana na Stoltenberg, njia pekee ya kufikia suluhisho  la haki na la kudumu ni kumshawishi Rais Putin kwamba hatashinda kwenye uwanja wa vita. Na njia pekee ya kuhakikisha kuwa Rais Putin anatambua kuwa hashindi kwenye uwanja wa vita ni kuendelea kuiunga mkono Ukraine kwenye mzozo wake na Urusi.

Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban amekuwa akipinga ufadhili kwa Ukraine na kuanzishwa kwa mazungumzo ya uanachama wa taifa hilo katika Umoja wa Ulaya.Picha: Yves Herman/REUTERS

Scholz asisitiza umuhimu wa kutuma ishara kwa Putin

Akizungumza alipowasili kwenye mkutano wa kilele wa mjini Brussels, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesisitiza kuwa uamuzi wa mkutano huo kuhusu Ukraine ni ishara muhimu kwa pande zote husika kwenye mzozo wa Urusi na Ukraine.

Zelensky ahimiza nchi wanachama wa EU na Marekani kuipa Ukraine misaada zaidi ya kifedha

"Na ndiyo maana ni muhimu pia kwamba ishara ya uungwaji mkono itumwe kwa raia wajasiri wa Ukraine, ambao wanatetea nchi yao, lakini pia ishara kwa rais wa Urusi, ambaye lazima ajue kuwa hawezi kutegemea Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wake ziache kuunga mkono Ukraine,” amesema Scholz.

Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orbán amesisitiza msimamo wake kwamba hakuna haja ya kuanzisha mazungumzo kuhusu kuiruhusu Ukraine kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Poland na Hungary zina tatizo la demokrasia

Viktor Orban amesema ni mapema sana kujadili hoja hiyo akidai kuwa Ukraine haijatimiza hata kanuni tatu miongoni mwa saba zilizowekwa na tume ya umoja huo.

Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: ALEXANDER ZEMLIANICHENKO/AFP/Getty Images

Putin: Urusi imewapeleka zaidi ya wanajeshi 600,000 nchini Ukraine

Kuhusu mpango wa Umoja wa Ulaya wa ufadhili kwa Ukraine jingine, Orban ameashiria kutolegeza msimamo wake licha ya umoja huo kuirudishia Hungary uwezo wa kupata dola bilioni 10 za miradi ya maendeleo. Orban amesema Hungary haihusishi masuala yake ya ndani na yale ya Ukraine. 

Hayo yakijiri, nchini Urusi, Rais Vladimir Putin amesema kuwa nchi yake imewapeleka zaidi ya wanajeshi 600,000 nchini Ukraine, karibu miaka miwili baada ya kuwaamuru wanajeshi wake kuuteka mji mkuu wa Kyiv.

Baada ya miezi ya mapambano, inaaminika kuwa wanajeshi wengi wa Urusi na Ukraine wameangamia. Marekani inaamini kuwa takriban wanajeshi 315,000 wa Urusi wameuawa au wamejeruhiwa.

Putin aliyasema hayo wakati wa mkutano wake wa mwisho wa mwaka na waandishi wa habari, na kuongeza kwamba hakukuwa na mipango ya haraka ya kuanzisha duru mpya ya uhamasishaji wa wanaume wa Urusi kujiunga na jeshi kwenye mzozo huo.

Vyanzo: AFPE, DPAE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW