1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schulz apitishwa kuwania ukansela dhidi ya Merkel

19 Machi 2017

Martin Shulz Jumapili (19.03.2017) amechaguliwa rasmi kugombea Ukansela dhidi ya Angela Merkel katika uchaguzi uliopangwa kufanyika hapo mwezi wa Septemba kumn'gowa mwanamke ambaye anatajwa kuwa shupavu kabisa duniani.

Deutschland SPD-Bundesparteitag in Berlin
Picha: Reuters/A. Schmidt

Mwanasiasa huyo wa chama cha Social Demokrat ambaye tayari anasifiwa kwa kukipa nguvu upya chama chake amechaguliwa kwa kauli moja kuwa kiongozi wa chama cha SPD na mgombea katika mkutano wa chama wa siku moja uliofanyika mjini Berlin.

Hotuba yake kwa viongozi na wanachama wa chama hicho  Schulz mwenye umri wa miaka 61 amejaribu kuimarisha kasi ya umashuhuri wake dhidi ya Merkel ambaye muungano wake wa kihafidhina miezi michache iliopita ulikuwa ukiongoza kusikopingika.

Ameuambia mkutano huo wa chama chake "kuanzia sasa mapambano ya kuwa chama kikuu yanaanza nchini kuuchukuwa Ukansela."

Pumzi mpya

Martin Shulz katika mkutano wa SPD Berlin. Picha: Reuters/F. Bensch

Uamuzi wa Shulz kuondoka bunge la Ulaya ambapo amekuwa akiliongoza kwa miaka mitano kama spika na kuwa ngonbea uongozi wa Ujerumani umekipa chama cha SPD  pumzi mpya tokea mkuu wa zamani wa chama hicho Sigmar Gabriel alipomtaka ashike hatamu za kukiongoza hapo mwezi wa Januari.

Shulz ameiambia radio ya umma ya Berlin RBB wiki hii "inatia moyo kuona kwamba katika wiki chache zilizopita watu wameanza kuwa na matumaini kwamba chama cha SPD kimepata nguvu kutaka ushindi wa uchaguzi.

Amesema ni dhahir kwamba nia yake ya kutaka kutekeleza sera ambazo zitaboresha kidogo hali ya maisha ya wachapa kazi imefanya watu wengi wamuunge mkono.

Uchunguzi wa maoni umeonyesha chama cha SPD kimejipatia pointi kumi katika wiki za hivi karibuni wengine wakikiweka mbele ya muungano wa kihafidhina wa Merkel ambaye anataraji kushinda muhula wa nne madarakani.

Chama cha SPD kimefytuwa risasi ya kwanza ya kuanza kampeni ya uchaguzi mkuu na pia uchaguzi wa majimbo matatu ya Ujerumani ambao wa kwanza utafanyika Saarland kwenye mpaka na Ufaransa hapo Machi 26.

Ameliambia gazeti la Bild Jumapili kwamba wote wawili yeye na Angela Merkel wana sifa za kuwa kansela.

SPD yachoshwa na serikali ya mseto

Martin Shulz katika mkutano wa SPD BerlinPicha: Reuters/A. Schmidt

Chama cha Social Demokrat washirika wadogo katika serikali ya mseto ya Merkel kwa takriban miaka minane kati ya kumi na mbili iliopita imekuwa chini ya kuvuli cha Merkel.Lakini Gabriel ambaye sasa ni waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani amewaambia wafuasi mwezi huu kwamba kuingia kwa Shulz katika kinyan'ganyiro hicho cha Ukansela akiwa mtu nje ya serikali kumewavutia wapiga kura wengi wa chama cha SPD ambao wamechoka kuwamo katika serikali ya mseto ya ya"muungano mkuu".

Historia ya Schulz ni ya aina yake alitaka kuwa mchezaji wakabumbu wa kulipwa,hakumaliza shule ya sekondari aliweza kuachana na tabia ya ulevi wa kupindukia na alifunguwa duka la vitabu na kujifunza lugha tano.

Wanachama wa chama chake wanatumai Shulz ataweza kuondowa mgawanyiko uliko kwenye chama hicho kutokana na mpango wa mageuzi ya soko la ajira unaojulikana kama Agenda 2010 uliopitishwa na kansela wa mwisho wa chama cha SPD Gerhard Schroeder ambaye alishindwa na Merkel hapo mwaka 2005.


Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : John Juma             

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW