1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schulz aungwa mkono zaidi na wapiga kura kuliko Merkel

Caro Robi
3 Februari 2017

Kura ya maoni inaonyesha mgombea Ukansela nchini Ujerumani wa chama cha Social Democratic SPD Martin Schulz atapata kura asilimia 16 zaidi dhidi ya Kansela wa sasa Angela Merkel wa Christian Democratic Union CDU.

Frankreich Angela Merkel und Martin Schulz in Verdun
Picha: Getty Images/S. Gallup

Chama cha SPD kimepata uungwajii mkono zaidi tangu Schulz kuteuliwa kuwa mgombea Ukansela wa chama hicho. Kura ya maoni iliyoendeshwa na shirika la vituo vya umma vya utangazaji nchini Ujerumani  ARD imefichua kuwa iwapo uchaguzi utafanyika leo, Wajerumani watamchagua Schulz kama Kansela.

Schulz atapokea asilimia 50 ya kura ilhali Merkel atapata asilimia 34. Hata hivyo Wajerumani ambao watashiriki katika uchaguzi wa bunge mwezi Septemba mwaka huu, hawatashiriki katika kumchagua Kansela moja kwa moja. Tangu kutangaza nia ya kugombea Ukansela mwezi uliopita, wanaomuunga mkono wameongezeka kwa asilimia 9 ilhali Merkel akishuhudia wanaomuunga mkono wakishuka kwa asilimia saba mwishoni mwa mwezi uliopita.

SDP chashamiri zaidi kisiasa

Matokeo hayo ya uchunguzi wa maoni yanaonyesha kuwa SPD, chama cha siasa za wastani za  mrengo wa kushoto, kimenufaika pakubwa kisiasa tangu kumteua Schulz Rais spika wa zamani wa bunge la Umoja wa Ulaya  kuwa mgombea wao.

Grafu inayoonyesha umaarufu wa vyama vya Ujerumani

Chama hicho kina uungwaji mkono wa asilimia 28 ya wapiga kura kote Ujerumani, huo ukiwa uungwaji mkono mkubwa kuwahi kushuhudia katika kipindi cha bunge la sasa kilichoanza mwaka 2013.

Licha ya kuongezeka huko kwa uungwaji mkono, CDU kinasalia kuwa chama imara zaidi cha kisiasa nchini Ujerumani kikiongoza kwa asilimia 34 kote nchini. Nusu ya walioshiriki katika kura ya maoni iliyoendeshwa an ARD wameelezea matamanio ya kutaka kukiona chama SPD kikichukua hatamu za uongozi wa serikali kuu kutoka kwa CDU na chama ndugu  cha Christian Social Union CSU cha jimbo la  Bavaria. Ni asilimia 39 tu ya waliohojiwa wanataka CDU na CSU kuendelea kuiongoza Ujerumani.

Matokeo mseto kwa vyama vidogo

Uchunguzi huo uliowahoji wapiga kura waliosajiliwa 1,506 kuanzia Jumatatu hadi Jumatano wiki hii unakuja miezi minane kabla ya uchaguzi ujao wa bunge unaopangiwa kufanyika tarehe 24 mwezi Septemba.

Chama kinachofuatiliwa kwa karibu cha Alternative Für Deutchland AfD ambacho kinafuata siasa kali za kizalendo za mrengo wa kulia, kuwapinga wahamiaji na ushawishi wa Uislamu Ujerumani, pia kimepiga hatua kisiasa katika nyanja za majimboni kikiungwa mkono kwa asilimia 12, hizo zikiwa alama tatu zaidi tangu kura ya mwisho ya maoni iliyofanywa mwezi uliopita.

Kiongozi wa chama cha AfD Frauke PetryPicha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Vyama vya kushoto ( die Linke)  na  kijani (Die Grüne) pia vimepoteza kila mmoja alama moja  tangu Januari na hivyo kuwaacha na asilimia 8 pekee ya uungwaji mkono.

Matokeo ya kura hiyo ya maoni  ni habari njema kwa chama cha Free Democratic FDP ambacho kimeshuhudia ongezeko la uungwaji mkono kwa alama moja zaidi na hivyo kukiweka katika asilimia sita  kikitumai  safari hii kupata fursa ya kurudi tena bungeni.

Chama hicho cha FDP hakijakuwa na uwakilishi bungeni tangu mwaka 2013, baada ya kupata asilimia 4.8  tu ya kura wakati huo na hivyo kushindwa  kifikia  asilimia 5 inayohitajika  kuweza kuwa na uwakilishi bungeni.

 

Mwandishi: Caro Robi/Dw English

Mhariri: Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW