1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scotland sasa kupiga kura ya maoni 2014

16 Oktoba 2012

Waziri Mkuu wa Uingereza na waziri kiongozi wa Scotland wameanza kampeni ya miaka miwili kuelekea kura ya maoni itakayoamua hatima ya Scotland kuendelea kubakia sehemu ya Uingereza au kujitenga na kuwa taifa huru.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, na Waziri Mkuu wa Scotland, Alex Salmond.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, na Waziri Mkuu wa Scotland, Alex Salmond.Picha: Reuters

Cameron na Salmond, anayetambulika kwa msimamo wake wa Scotland huru, walisaini makubaliano na kupeana mikono hapo jana katika jengo la Mtakatifu Andrew, makao makuu ya serikali ya Scotland, mjini Edinburgh, kila mmoja akiwa na msimamo wake.

Cameron anapingana vikali na kujitenga kwa Scotland baada ya zaidi ya miaka 300 ya Muungano na Uingereza, wakati Salmond akiamini kwamba wakati wa Scotland kuwa huru sasa umewadia na kwamba kura ya mwaka 2014 itasafisha njia kwa uhuru huo.

"Hii ni historia. Nina fahari kwamba nimeishi nikitimiza wajibu wangu wa kihistoria. Kwa hakika ni siku kubwa leo, siku kubwa kwa Scotland lakini baadaye tuna miaka mingi migumu ijayo kuinusuru hatima ya taifa hili." Amesema Salmond.

Kazi ngumu yaanza

Hatua hii iliyofikiwa baada ya miezi kadhaa ya majadiliano, peke yake ni ushindi wa awali kwa mwanasiasa huyo mkongwe wa Scotland, ambaye ameutumia umri wake wote wa kisiasa kupigania Scotland huru, lakini ambaye anakabiliwa na kikwazo kikubwa cha kuweza kuishawishi sehemu kubwa ya wakaazi wa Scotland kuunga mkono msimamo wake kwenye kisanduku cha kura.

Malkia Elisabeth II wa Uingereza akiwa ziarani kwa mara ya mwanzo huko Scotland tarehe 8 Agosti 2011.Picha: picture-alliance/dpa

Uchunguzi wa maoni ya wananchi uliotangazwa jana, unaonesha kuwa ni asimilia 34 tu wa wakaazi wa Scotland na asilimia 29 ya Waingereza wote wanaotaka Scotland ijitenge.

Hata hivyo, Salmond aliwaambia waandishi wa habari kwamba baada ya kusaini makubaliano hayo, matokeo ya uchaguzi mkuu wa Mei 2011, ambayo yalikipa chama chake cha Kizalendo, SNP, wingi wa kura bungeni, ndiyo yaliyofungua mlango wa kura ya maoni.

Cameron hatawazuia Waskoti kuwa huru

Cameron amesema kwamba alisema licha ya kuwa ni muhimu sana kwa Uingereza kuwa moja daima, lakini hawezi kulazimisha nchi kubakia kuwa sehemu ya Uingereza ikiwa matakwa ya wananchi wake ni kinyume.

Bendera ya Scotland.Picha: AP

"Kwa moyo wangu wote naamini kwamba Scotland itakuwa njema zaidi ndani ya Uingereza, lakini la muhimu zaidi ni kuwa Uingereza itakuwa bora zaidi ikiwa na Scotland. Kwa pamoja, tuko bora zaidi. Kwa pamoja, tuna nguvu zaidi. Kwa pamoja tuko salama zaidi. Tuko bora zaidi tukiwa pamoja. Wacha hoja sasa zitolewe, na natarajia watu watapiga kura ya kuendelea kuiweka Uingereza pamoja."

Salmond ameyaita makubaliano hayo ya Edinburgh kama "njia safi kwa maamuzi muhimu kabisa kuwahi kufanywa na Scotland katika karne kadhaa."

Chama cha SNP sasa kina kazi ya kupambana na vyama vyote vitatu vikubwa kwenye mabaraza ya Bunge la Uingereza, kikiwemo cha Kihadifhina cha Waziri Mkuu Cameron, mshirika wake, chama cha Kiliberali, na chama kikuu cha upinzani cha Labour, ambavyo vyote vinapinga Scotland kujitenga.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW