Seehofer aunga mkono Bundesliga irejee viwanjani
3 Mei 2020
"Naona ratiba iliyopendekezwa na kitengo cha ligi kinachopanga ratiba ya mechi inatekelezeka na naunga mkono Bundesliga irejee tena viwanjani Mei," Horst Seehofer aliliambia gazeti la Bild, siku tatu kabla kufanyika mkutano wa maafisa wa Ujerumani utakaolijadili suala hilo.
Bodi ya ligi, DFL, unaunga mkono kuanza tena kwa mechi za Bundesliga bila mashabiki uwanjani katikati ya Mei, hatua itakayoifanya ligi hii kuwa ya kwanza kubwa ya Ulaya kupitisha uamuzi wa aina hiyo.
Seehofer, ambaye ana dhamana na jukumu muhimu la serikali kuhusiana na suala hilo kwa kuwa ana vyeo kadhaa, amesisitiza kuwa timu na wachezaji lazima waheshimu masharti kadhaa.
"Iwapo kutathfibitika kisa cha maambukizi ya corona katika timu au uongozi wa timu, klabu yote, na hata timu waliyocheza dhidi yao mwisho, lazima waende katika karantini kwa wiki mbili," alisema.
"Kutaendelea kwa hivyo kuwepo hatari kwa ratiba ya mechi na kwa kazi ya kupanga ratiba," iwapo kutakuwepo maambukizi.
Lakini Seehofer alisema vilabu havitakuwa na fursa maalumu ya kufanyiwa vipimo ambayo umma wote umenyimwa. Timu kadhaa zimependekeza kufanya vipimo mara kwa mara kwa wachezaji wao kama hatua ya kuzuia maambukizi ya kirusi cha corona.
(afpe)