1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya kwanza ya Ramadhani kwa mataifa kadhaa duniani

11 Machi 2024

Saudi Arabia, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu zimetangaza kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, katika kipindi ambacho kimegubikwa na hali mbaya ya kiutu huko Ukada wa Gaza.

Bangladesch Eid al-Fitr
Waislamu wa Bangladesh wasali sala ya Eid al-Fitr, huko Dhaka mnamo Aprili 22, 2023.Picha: Munir Uz Zaman/AFP

Saudi Arabia, ambayo ni sehemu ya maeneo matakatifu zaidi ya Uislamu, ilisema jana Jumapili (10.03.2024) kupitia shirika lake la habari SPA kwamba Mahakama ya Juu imetangaza "Jumatatu, Machi 11, 2024, kuwa ni mwanzo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mwaka huu".

Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar pia zilitangaza tarehe hiyo kuanza kwa Ramadhani kupitia vyombo vyao rasmi vya habari baada ya mwanandamo wa mwezi.

Ramadhani ni moja kati ya nguzo tano za Uislamu

Baraza la ushauri la Kiislamu la Misri Dar al-Ifta pia lilithibitisha kuwa Ramadhani itaanza Jumatatu,(11.12.2024) kama itakavyokuwa katika maeneo mengine ya Palestina ikijumuisha Gaza, Algeria na Tunisia.

Waislamu wa Bangladesh wasali sala ya Eid al-Fitr, huko Dhaka mnamo Aprili 22, 2023.Picha: Munir Uz Zaman/AFP

Majirani zao Morocco na Libya walisema Ramadhani itaanza Jumanne. Lakini pia awali kabisa, Iran ilitangaza kuwa mwanzo wa Ramadhani utakuwa Jumanne hiyo baada ya ofisi yake yenye dhima ya uchunguzi wa mwezi kusema haikuwezekana kuanza kwa kile kilichoelezwa kutoshuhudiwa kwa mwandamo wa mwezi.

Mashaka ya mwandamo wa mwezi Saudi Arabia

Huko Saudi Arabia, kuanza kwa mwezi mtukufu kulitiliwa mashaka baada ya baadhi ya vyombo vya uchunguzi vya ufalme huo kuripoti kwamba mwezi ulifichwa na "hali ya hewa ya mawingu na chembe za vumbi". Lakini uthibitisho wa mwisho wa muandamo huo ulitolewa kupitia Chuo Kikuu cha Al Majmaah cha huko Riyadh.

Oman pia itaadhimisha siku ya kwanza ya Ramadhani Jumanne. Katika kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani waumini wa dini ya Kiislamu hujizuia kula na kunywa kuanzia alfajiri hadi jioni, na kwa desturi hukusanyika pamoja na familia na marafiki ili kufuturu katika nyakati za jioni.

Pia ni wakati wa sala, ambapo waumini hukusanyika kwa wingi misikitini, haswa nyakati za usiku.

Soma ziadi:Wapalestina kuanza Ramadhan katika kivuli cha vita Gaza

Vita kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza vimeleta giza nene kwa mwezi huu mtukufu kwa waumini wa dini ya Kiislamu katika eneo hilo, huku matumaini  ya amani yakiwa yamefifia na hasa baada ya kushindwa kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano kabla ya mwezi wa Ramadhani kuanza.

Chanzo: AFP