1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Senegal kuanzisha uchunguzi baada ya machafuko

8 Juni 2023

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ametoa wito wa kuheshimiwa kwa demokrasia nchini Senegal baada ya kuibuka kwa mapigano ya nadra baada ya kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko kutiwa hatiani.

Frankreich Senegalese diaspora protest - Paris
Picha: Prezat Denis/Avenir Pictures/abaca/picture alliance

Katika mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Macky Sall, Blinken alitoa salamu za rambirambi baada ya takriban watu 16 kuuawa katika machafuko hayo.

Soma pia: Senegal: Utulivu warejea baada ya maandamano yenye ghasia

Ghasia hizo zilizuka wiki iliyopita baada ya kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko, mkaguzi wa zamani wa kodi ambaye amepata umaarufu miongoni mwa vijana kwa kuzungumza dhidi ya umaskini na ufisadi, kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.

Sonko alihukumiwa kwa kumdhalilisha kingono mwanamke mmoja baada ya kukwepa shtaka kubwa zaidi la ubakaji.

Akiwa katika ziara ya siku tatu nchini Saudi Arabia Blinken, kupitia mtandao wa Twitter amesisitiza kwamba Marekani itaendelea kuwaunga mkono watu wa Senegal na maadili ya kidemokrasia.

Mnamo mwaka 2021 Blinken alisafiri hadi Senegal katika safari yake ya kwanza barani Afrika kama mwanadiplomasia mkuu wa Marekani, akiangazia rekodi thabiti ya kihistoria ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi kuhusu demokrasia wakati China inapanua ushawishi barani Afrika.

Uchunguzi zaidi

Picha: Presidency of Senegal / Handout/AA/picture alliance

Huku haya yakijiri Serikali ya Senegal imesema imeanzisha mara moja uchunguzi kuhusu vurugu zilizozuka nchini humo na kusababisha vifo vya takriban watu 16 na mamia kujeruhiwa.

Soma pia: Mpinzani mkuu Senegal akabiliwa na kesi ya ubakaji

Taarifa ya serikali imeendelea kusema kuwa uchunguzi huo utabaini wale waliohusika huku ikilaani kile ilichokiita "mashambulizi makali dhidi ya serikali, jamuhuri na taasisi" na kusema ghasia hizo zililenga kuchochea ugaidi na kuilemaza nchi hiyo.

Aidha Rais Macky Sall ameitaka serikali kuchukua hatua kusaidia watu na mashirika ambayo yamepata madhara.

Doudou Diene, mmoja wa wahanga wa ghasia hizo amezikwa na wazazi wake wanaodai kuwa mtoto wao aliuawa kwa kupigwa risasi na sasa wanadai "haki itendeke".

"Haki itendeke kwa sababu watu wasio na hatia wanakufa na sio kawaida. Unaona, mtoto aliyemwacha mwenye umri wa mwaka mmoja, mke aliyemuacha, na ndoto zake." alisema mama yake Doudou.

Makabiliano kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa Sonko yalizuka Juni mosi baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili katika kesi anayosema ilibuniwa ili kumzuia kuwania urais katika uchaguzi wa mwakani.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW