Senegal ndio Fahari ya Afrika katika kombe la Dunia
22 Juni 2018Kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Poland siku ya Jumanne, Senegal ilijidhihirisha kama timu yenye nidhamu. Kivutio kikubwa lakini ni mashabiki wa Senegal kwani ni mfano wa kuigwa. Mhariri wa Süddeutsche Online alisema mashabiki wote wa soka wanatakiwa wajifunze kutoka kwa mashabiki wa Senegal. Kocha wa Senegal Aliou Cissé amenukuliwa akisema bara zima la Afrika linawaunga mkono, mashabiki wana fahari na timu yake.
Haikuwa mechi ya Robert Lewandowski, ambaye aliugusa mpira mara 34, bali ilikuwa ni ya Senegal, timu ya kwanza kutoka Afrika kupata ushindi katika mashindano ya kombe la dunia, Urusi.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema "Senegal ni Fahari ya Afrika". Chini ya kocha ya Aliou Cissé Senegal ilifaulu kufanya kile ambacho timu nyingine kutoka barani Afrika zimeshindwa kukifanya.
Mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine akaendelea kuandika kuwa Afrika ilikuwa imesahaulika katika ulimwengu wa soka, lakini ushindi wa Senegal dhidi ya Poland umeamsha hisia na kuwakumbusha mashambiki katika bara zima la Afrika kwamba matumaini yangalipo. Kocha Aliou Cissé alinukuliwa na gazeti hilo akisema Senegal inaliwakilisha bara zima la Afrika katika mashidano ya Urusi.
Ukusanyaji kodi kutumia vifaa vya kielektroniki
Mada ya pili iliyozingatiwa na magazeti ya Ujerumani ni ukusanyaji wa kodi nchini Tanzania. Gazeti la Neue Zürcher liliandika kuhusu wakusanyaji kodi wanaotegemea vifaa vya kielektroniki, kama vile vinavyotumiwa kusomea data za kadi za benki.
Mhariri wa gazeti la Neue Zürcher alisema vifaa hivyo vimeenea nchini Tanzania katika muongo mmoja uliopita. Serikali inapania kukusanya kodi zaidi. Mataifa mengi ya Afrika yanakabiliwa na changamoto nyingi katika ukusanyaji wa kodi katika sekta isiyo rasmi, huku mengi yakitumia viwango vikubwa vya fedha kuliko zile zinazokusanywa. Kenya na Malawi zinatumia mfumo wa ukusanyaji kodi ya mauzo kwa njia ya kielektroniki kwa muda mrefu. Ghana nayo itaanzisha hivi karibuni. Mhariri anaonya uwezekano bado upo wa kukwepa kulipa kodi licha ya vifaa hivi. Aliyezowea kukwepa, atakwepa tu katika siku zijazo kwa kuwa vifaa havizibadili fikra wala mtazamo.
Kambi ya wakimbizi ya Dadaab ni jela ya wazi
Gazeti la Süddeutsche Online liliandika kuhusu kambi kubwa ya wakimbizi duniani ya Dadaab nchini Kenya. "Daadab ni gereza la wazi" ndivyo alivyoandika mhariri wa gazeti hilo.
Kambi ya Dadaab nchini Kenya imefahamika kama kambi kubwa kabisa ya wakimbizi duniani ambako wakimbizi nusu milioni wanaishi, wengi wao wakitokea taifa jirani la Somalia, ambako walikimbia vita na machafuko. Gazeti lilichapisha mahojiano na mkimbizi wa kisomali Hussein Mohammud, almaarufu Suud Olat, aliyeanza kuishi katika kambi hiyo akiwa na umri wa miaka sita, lakini sasa anaishi katika jimbo la Minnesota nchini Marekani baada ya kusaidiwa kusafiri na shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi la UNHCR.
Hussein anasema huko Dadaab mtu huishi katika jamii isiyo na ajira, huduma za afya ni mbaya, chakula ni kichache, hakuna uhuru na matumaini ya maisha ya neema ni finyu. Mkimbizi huyo ambaye sasa ana umri wa miaka 27 anasomea taaluma ya utengenezaji filamu na mawasiliano katika chuo kikuu cha Minnesota, na ni mwanachama wa asasi isiyo ya kiserikali ya Film Aid International, inayotayarisha video, kuhusu na kwa ajili, ya watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao.
Vita vya Congo vyailekeza wapi nchi?
Gazeti la Süddeutsche Zeitung liliripoti juu ya machafuko yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Gazeti lilisema baada ya miongo kadhaa mapigano yamekuwa yakiendelea bila msaada wowote wa maana kutoka nje. Lakini je, hali hii inalielekeza wapi taifa la Congo? Mhariri akauliza na kuendelea kueleza:
Congo ni nchi ambayo karibu nusu ya idadi jumla ya wakazi wake milioni 80 wana umri wa chini ya miaka 14. Wengi wao ni wahanga wa vita ambavyo vimedumu miaka mingi kuliko umri wao. Ni watoto wa vita ambao ulimwengu umeshawazika katika kaburi la sahau. Mhariri anasema ni hali ya kutatanisha, ya kukatisha tamaa, na Congo kunachukuliwa kuwa ni mbali sana. Ni nchi ambayo imepoteza udhibiti wa himaya yake. Serikali ya mjini Kinshasa iliususia mkutano wa wafadhili uliofanyika mjini Geneva, Uswisi mwezi Aprili mwaka huu, ambao ulitakiwa kuchangisha fedha kwa ajili ya raia kiasi milioni 13 wa Congo, ambao hawawezi tena kuyasimamia mahitaji yao. Mhariri anasema serikali haikujali.
Mvutano kati ya nchi za Ghuba wafika Somalia
"Mgogoro wa eneo la Ghuba unaiangamiza Somalia" hivyo ndivyo lilivyoandika gazeti la Neue Zürcher katika taarifa yake. Mhariri ameandika juu ya kisa cha ndege kutoka Abu Dhabi iliyopeleka masanduku matatu Somalia. Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu UAE hakutaka yachunguzwe kupitia mashine za picha kabla kutoka uwanja wa ndege na badala yake akayarudisha ndani ya ndege. Maafisa wa usalama wa Somalia wakatoa silaha zao na kuyachukua masanduku hayo na ndani wakapata kiasi faranga milioni kumi fedha taslimu.
Kisa hicho kilichotokea mwezi Aprili kilidhihirisha mahusiano ya kutia mashaka kati ya Somalia na Emarati. Somalia inashuku fedha hizo zilinuiwa kuidhoofisha serikali, lakini Emarati inasema zilitakiwa kutumika kulipa mishahara ya wanajeshi wa Somalia. Ukweli kuhusu kadhia hiyo haujabainika. Mhariri wa gazeti la Neue Zürcher alisema Somalia sio taifa lililoshindwa linalowategemea wafadhili.
Kutokana na eneo ilipo kijiografia na masilahi ya kiuchumi, nchi za ghuba hususan Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu, zimevutiwa sana na nchi hiyo katika miezi ya hivi karibuni. Lakini kwa kuwa Emarati imejaribu kwa mwaka mzima, kupitia msaada wa Saudi Arabia, kuitenga Qatar kwa madai ya kufadhili ugaidi, nchi hizo jirani zimekuwa zikilumbana. Na mgogoro huu umesababisha vita vya kung'ang'ania ushawishi nchini Somalia pia kwa kuwa Qatar inaiunga mkono serikali ya Somalia mjini Mogadishu huku Emarati ikiliunga mkono jimbo lenye utawala wake wa ndani la Somaliland.
Mwandishi: Josephat Charo/Pressedatenbank
Mhariri: Mohammed Khelef