1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Senegal yajiandaa kwa uchaguzi wa kihistoria wa rais

23 Machi 2024

Senegal inafanya uchaguzi wa rais Jumapili ya Machi 24, 2024 baada ya sarakasi za majuma kadhaa yaliyoshuhudia machafuko kufuatia tangazo la hapo kabla la kuahirishwa uchaguzi huo.

Shamra shamra za wakati wa kampeni
Shamra shamra za wakati wa kampeni Picha: SEYLLOU/AFP

Rais Macky Sall anayemaliza muhula wake wa pili, aliushangaza ulimwengu pale alipotangaza kuuahirisha uchaguzi wa rais uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 25.

Mara moja tangazo lake lilizusha ukosoaji na maandamano ya umma yaliyosababisha vifo vya watu 4.

Baada ya shinikizo la ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na uamuzi wa Mahakama ya Katiba, rais Sall alitangaza tarehe mpya ya uchaguzi ya Machi 24.

Mnamo siku ya Ijumaa, wagombea wa kiti cha urais walifanya mikutano ya mwisho ya kampeni zilizofanyika kwa kipindi kifupi na bila matayarisho ya kutosha kutokana na mparaganyiko ulifuatia kuahirishwa kwa uchaguzi.

Watu milioni 7 wanayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi huo wa Jumapili, kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi linalosifika kwa utulivu wa kisiasa na ambalo linatazamiwa mwaka huu kuanza kuwa mzalishaji wa mafuta.

Hata hivyo zaidi ya theluthi ya umma wa Senegal ni masikini na nusu ya raia wake ni vijana walio na umri wa chini ya miaka 20.

Wagombea 17 wanachuana kumrithi rais Macky Sall

Mgombea urais kwa tiketi ya chama tawala nchini Senegal, Amadou Ba (kushoto) akiwa na rais anayemaliza muda wake Macky SallPicha: SEYLLOU/AFP/Getty Images

Baada ya wagombea wawili kujitoa kutoka kinyang´anyiro hicho mnamo dakika za lala salama, uchaguzi huo umesalia na wagombea 17 wanaowania kurithi kiti cha urais kutoka kwa Macky Sall.

Mshindi wa uchaguzi huo atakuwa na kibarua kikubwa cha kuitoa nchi hiyo kipindi cha msukosuko kilichoshuhudiwa miaka ya hivi karibuni lakini kuweka mpango wa kuinufisha Senegal kutokana na mapato ya nishati ya mafuta na gesi yanayotazamiwa kuanza kupatikana.

Wagombea wawili, wote maafisa wa zamani wa masuala ya kodi, ndiyo wanapigiwa upatu wa kupata ushindi -- mgombea wa chama tawala na waziri mkuu wa zamani Amadou Ba, na mgombea wa upinzani Bassirou Diomaye Faye.

Faye alitolewa gerezani wiki iliyopita, ikiwa imepita wiki moja tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi, akiwa pamoja na mwanasiasa mwengine mashuhuri  Ousmane Sonko, ambaye hata hivyo amezuiwa kushiriki uchaguzi huo. Sonko badala yake anamuunga mkono Faye.

Mgombea mwengine aliondolewa kwenye uchaguzi huo kwa kutotimiza sifa Karim Wade, mtoto wa rais wa zamani Abdoulaye Wade, aliwaambia wafuasi wake siku ya Ijumaa wamuunge mkono Faye. Tangazo hilo limeuongezea nguvu upande wa upinzani kuelekea uchaguzi huo.

Kampeni za mwisho mwisho na matarajio ya wapiga kura

Mgombea kigogo wa upinzani nchini Senegal, Bassirou Diomaye Faye.Picha: AFP via Getty Images

Mnamo Ijumaa, maelfu ya wafuasi wa Faye wakiwa wamebeba picha za mwanasiasa huyo walikusanyika kwenye mji wa magharibi wa Mbour, kwa mkutano wa mwisho wa kampeni.

Kwenye uwanja wa Place de la Nation uliopo kwenye mji mkuu, Dakar, mamia ya wafuasi wa Amadou Ba nao walikusanyika kumsikiliza mgombea huyo.

"Tunafahamu kuwa hawa wawili ndiyo watakaoshinda iwapo hakuna balaa lolote litakalojitokeza," amesema El Hadji Mamadou Mbaye, mhadhiri wa sayansi ya siasa na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Saint-Louis, akiwazungumzia Ba na Baye.

Ushindi wa Faye utakuwa ni "mtikisiko" wa kisiasa, anasema Mbaye, kutokana na ukweli kwamba mwanasiasa huyo siyo sehemu ya tabaka linalotawala nchini Senegal. Matokeo ya uchaguzi yanatizamiwa kuanza kutolewa Jumapili usiku.

Iwapo uchaguzi wa Jumapili hautatoa mshindi wa moja kwa moja, duru ya pili itaandaliwa lakini tarehe yake bado haijatangazwa.

Macho ya walimwengu yataimulika kwa ukaribu Senegal

Takwimu zinaonesha asilimia 39 ya raia milioni 18 wa Senegal wanaishi kwenye umasikini.Picha: Muhamadou Bittaye/AFP/Getty Images

Washirika wa kimataifa watakuwa wakiufuatilia uchaguzi huo kwa ukaribu. Hali ya maisha kwenye nchi hiyo ya raia milioni 18 imezidi kuwa mbaya miaka ya karibuni. Asilimia 39 ya wakaazi wake wanaishi kwenye dimbwi la umasikini.

Takwimu hizo ni kulingana na Shirika linalosimamia mpango wa utoaji Misaada ya Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP.

Hali hiyo ya kiuchumi imewalazimisha vijana wengine kuikimbia Senegal wakitumia boti za mpira na mitumbwi kujaribu kuingia Ulaya.

Kwa miaka mingi Senegal imekuwa inazingatiwa alama ya utulivu kwenye kanda ya magharibi mwa Afrika iliyogubikwa na mapinduzi ya kijeshi ya kila wakati.

Nchi hiyo imekuwa na mahusiano mazuri na mataifa ya magharibi hata katika wakati mataifa jirani ya kanda ya Sahel yamebadili mkondo kuelekea Urusi.

  

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW