SEOUL: Majadiliano kuregeza masharti ya utandawazi
7 Mei 2007Korea ya Kusini na Umoja wa Ulaya hii leo zinaanzisha majadiliano kuhusika na biashara huru.Pande zote mbili zimesema,makubaliano yataimarisha biashara ya pande hizo mbili na kusaidia juhudi za kuregeza masharti ya biashara duniani.Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Seoul,waziri wa biashara wa Korea ya Kusini Kim-Hyun Chong alisema,hii ni nafasi nzuri kwa Korea ya Kusini kuwa kituo cha biashara huru cha Asia ya Mashariki,na kuunganisha pamoja Ulaya, Asia na Marekani.Tume zinazoanzisha majadiliano hayo zinakutana mjini Seoul kuanzia leo hadi Mei 11 kwa duru ya mwanzo ya mazungumzo.Umoja wa Ulaya ni mwekezaji mkubwa kabisa nchini Korea ya Kusini.Mwezi uliopita,Korea ya Kusini ilitia saini makubaliano muhimu ya biashara huru pamoja na Marekani.