Septemba 11, siku dunia ilipobadilika
9 Agosti 2011Miaka 10 baadaye, kinachoonekana ni kwamba hakuna kilichobadilika. Umoja wa Mataifa huko Marekani unatwikwa dhamana ya yote yanayoikabili dunia. Ujerumani inajishughulisha na mambo yake binafsi. Kuuliwa kwa Osama Bin Laden chini ya mpango ulioongozwa na majeshi ya Marekani ni jambo lililoibua sauti kutoka kila pembe. Na juu ya hilo, miaka 10 baada ya kutokea mashambulizi hayo mabaya kabisa ya kigaidi katika historia, wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanahisi hakuna siku inayotazamwa kuwa mbaya kabisa duniani kama tarehe 11 Septemba 2001, ambayo iliubadilisha kabisa ulimwengu.
Ilikuwa ni siku iliyowafanya watu kukosa uwezo wa kujisaidia, mauaji makubwa ya binadamu na janga kuu la kihistoria. Aidha ni tukio lililosumbua fikra na kuleta mitazamo potofu ya kisiasa na kiimani. Kwa hakika, tukio hili ulikuwa mwanzo wa kile kinachofuatia.Tarehe hiyo ni siku iliyothibitisha mpasuko katika fikra za walimwengu juu ya dunia kuhusu,mitazamo na nadharia za kisiasa. Madhila mengi yaliyotokana na mashambulizi hayo hadi hii leo hayajaweza kufidiwa.
Jambo la uhakika kwa upande wa nchi za Magharibi, ni kwamba katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, zimekuwa mara nyingi zikijikuta kuingiwa na wasiwasi na kuonyesha hali ya kuelemewa pamoja na kujitolea kuweka wazi mkakati wa kukabiliana na itikadi kali za kigaidi na kuwasiadia wanaopambana na ugaidi. Mfano ulio wazi kabisa ni juu ya matukio mabaya yaliyotokana na kuchapishwa kwa vikatuni vya kumkejeli Mtume Muhammad (S.A.W). Na zaidi hali hiyo imeongezeka nguvu hasa nchini Ujerumani kukiibuka mjadala ikiwa kuuliwa kwa mtu aliyesababisha vifo vya maelfu ya watu kama Osama Bin Laden, na aliyeichafulia jina itikadi na dini ya Kiislamu kunaweza kuleta hali ya maridhiano kimataifa.
Mjadala kama huo unaonyesha ni kwa jinsi gani nguvu za mashambulizi ya Septemba 2001 zilivyoutikisa mfumo mzima wa nchi za Magharibi. Mijadala hiyo inaonyesha jinsi gani mashambulizi ya Septemba 2001 yalivyoyatikisa maadili ya nchi za Magharibi. George W. Bush, ambaye bila shaka si miongoni mwa marais wanaosifika wa Marekani, alisema siku mbili tu kabla ya mashambulizi hayo ya kigaidi kwamba: "Sisi ndiyo uhuru pamoja na kila yaliyo mema. Kwa hiyo tuyalinde." Matamshi haya mepesi lakini muhimu, sasa yamepoteza maana unapoyaangalia matukio ya gereza la Guantanamo, Abu Ghraib na vifo vya maelfu ya watu vilivyotokana na vita dhidi ya ugaidi. Umuhimu wa msimamo ule sasa unaanza kuwa dhaifu. Hali hii inawabeza wahanga wa Septemba 11 na wale wa Kituo Kikuu cha Kibiashara Duniani (World Trade Center) ambao walilazimika kuchagua ama wafe ndani au wajitupe kutoka umbali wa mita 400 kujaribu kujinusuru.
Pamoja na hayo, mtazamo wa sura ya uongozi wa Bush ni: Kimsingi Afghanistan sasa imekuwa sio tena ngome kuu ya wenye itikadi kali kama ilivyokuwa awali. Iraq imeepukana na dikteta na imo katika njia ya kuelekea kwenye demokrasia. Na mapinduzi katika Mashariki ya Kati ni jambo lenye uwezekano. Na hayo yote ni matokeo yaliyo wazi yenye kujirudia mara kawa mara kwa lengo la kujitolea kwa ajili ya demokrasia na uhuru.
Ugaidi hauwezi kukubaliwa. Lakini pia lugha mbadala ya kulipiza kisasi kwa matumizi ya nguvu, kama inavyotafsiriwa na baadhi ya wanaoiunga mkono. Mwangaza wa habari wa Deutsche Welle unaonyesha hayo katika sura zote zinazohusiana na matukio yanayowahusu watu katika maeneo yote na pia kuhusiana na matumaini ya kila mmoja wetu, ikiwa ni miaka 10 baada ya Septemba 11 - siku iliyoibadili dunia.
Mwandishi: Marc Koch/ZPR
Tafsiri: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman