1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sera ya Marekani kuhusu Mashariki ya Kati itabadilishwa?

19 Januari 2021

Rais Trump amebaki na siku moja tu akiondoka Madarakani. Hatua za dakika za mwisho za utawala wake nchini Yemen, Iraq na Afrika Kaskazini zimekosolewa vikali. Ni jinsi gani maamuzi hayo yanaweza kubatilishwa kwa haraka?

Jemen Hilfe Katastrophenhilfe Flüchtlinge Flucht
Picha: AHMAD AL-BASHA/AFP/Getty Images

Zaidi ya wiki mbili zilizopita, utawala unaoondoka wa Trump umefanya maamuzi ya haraka ya kuimarisha mipango ya sera yake ya kigeni katika Masharikii ya Kati. Wiki iliyopita, Marekani iliwaorodhesha waasi wa Houthi nchini Yemen wanaoegemea Iran kuwa kundi la kigaidi na kumuwekea vikwazo afisa wa kijeshi wa Ira na mashirika kadhaa ya Iran. Desemba, ililitambua eneo linalogombaniwa la Sahara Magharibi kuwa himaya ya Morocco.

Soma pia: Mzozo wa Sahara Magharibi wafukuta

Hatua hizi zote zimetumika kuitenga Iran na kuimarisha Israel katika kanda hiyo, hatua ambazo wapiga kura wengi wa Marekani huenda wakakubaliana nazo. Lakini pia maamuzi hayo ya karibuni yamekosolewa vikali. Lakini utawala unaoingia wa Biden utaweza kuyabatilisha maamuzi hayo ambayo yanasemekana kuwa na madhara makubwa, na je, itachukua muda gani na mchakato utakuwa mgumu kiasi gani?

Wakimbizi katika kambi ya Smara ya Sahara MagharibiPicha: Louiza Ammi/abaca/picture alliance

Siku moja tu inayohitajika kufanya mabadiliko

Marina Henke, profesa wa mahusiano ya kimataifa katika Taasisi ya Hertie, mjini Berlin, anasema kinadharia, baadhi ya mabadiliko yanaweza kuwa rahisi tu. Kiufundi, mengi yanaweza kufanyika katika siku moja.

Kwa mfano uamuzi kuhusu Morocco na Sahara Magharibi ulikuwa katika aina ya tangazo lililofanywa na Trump. Halina nguvu za kisheria isipokuwa kama Bunge la Marekani litaidhinisha na linaweza kubatilishwa kwa urahisi na tangazo jingine kutoka kwa rais mpya. Amri za rais matamko hufanya kazi katika njia hiyo hiyo. Yanaweza kufutwa na hivyo hivyo na rais ajaye Joe Biden.

Kulitangaza kundi Fulani kuwa la kigaidi ni kitu kigumu, lakini sio sana. Waziri wa Mambo ya kigeni lazima atangaze nia yake ya kufanya hivyo, kisha bunge lina siku saba kuwasilisha malalamiko yoyote. 

Tayari kuzungumza na magaidi?

Henke anasema Waziri anayeondoka wa Mambo ya Kigeni Mike Pompeo ametengeneza dhana kuhusu masuala tete ya sera za kigeni yenye umuhimu kwa wapiga kura wa Marekani. Masuala yanayoihusisha Iran, China na Cuba. Na kama Biden atachukua hatua za haraka, Warepublican wanaweza kulalamika kuwa ana nia ya kuzungumza na magaidi.

Anthony Blinken ateuliwa Waziri wa mambo ya kigeniPicha: Chandan Khanna/AFP/Getty Images

Mahusiano ya nchi za Kiarabu na Israel yanaungwa mkono na pande zote

Lakini huenda kukawa na baadhi ya sera za kigeni zilizowekwa na Utawala wa Trump ambazo uongozi mpya wa Marekani haungependa kuzifuta. Julian Barnes-Dacey, mkurugenzi mtendaji wa mpango wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Baraza la Ulaya kuhusu Mahusiano ya Kigeni. Kuanzishwa mahusiano ya nchi za Kiarabu na Israel ni kitu ambacho kinaungwa mkono na pande zote za kisiasa. Kuhusu hali ya kiutu nchini Yemen, Biden huenda akajaribu kutafuta mbinu ya suala hilo badala ya kulikabili moja kwa moja.

Soma pia: Bahrain, UAE zaweka mahusiano ya kidiplomasia na Israel

Profesa wa masuala ya usalama katika Chuo Kikuu cha Massachussettes Lowell nchini Marekani anasema yote hayo yanahusu dhamira ya kisiasa. Amri za rais zinaweza kutolewa na kutekelezeka haraka. Bunge halihitaji kuhusika. Hata hivyo kama unazungumzia mataifa kama vile Iran au Syria, au baadhi ya wahusika nchini Iraq – hilo litakuwa suala gumu.

Muda unayoyoma kuhusu Iran

Ian Black, msomi mwandamizi katika Kituo cha Mashariki ya Kati cha Chuo cha Masuala ya Kiuchumi mjini London anasema suala muhimu ni kurejea katika mkataba wa nyuklia wa Iran. Anasema shinikizo kuhusu suala hilo ni kubwa mno, hata ingawa utawala wa Trump ulifanya kazi kubwa kuyaunganisha mataifa ya Ghuba na Israel dhidi ya Iran. Watalaamu tayari wameonya kuwa muafaka wa Iran utachukua muda kufufuliwa.