Sera ya wahamiaji bado kizaazaa Ujerumani
19 Juni 2018Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wameandika zaidi kuhusu mgogoro wa sera ya uhamiaji uliopo kati ya chama cha kansela Merkel cha Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union CSU kinachoongozwa na Horst Seehorfer ambaye pia ni waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani. Kadhalika wahariri wameandika juu ya kukamatwa kwa mkuu wa kampuni la magari la Audi kufuatia kadhia ya udanganyifu katika majiribio ya kupima viwango vya utoaji moshi wa magari.
Gazeti la Sächsische Zeitung» la (Dresden)
Kwa namna yoyote ile kwa hivi sasa Kansela Merkel na waziri wake wa mambo ya ndani wanatafautiana, kwamba polisi ya Ujerumani iwazuie toka sasa wakimbizi waliokataliwa kurejea nchini. Raia wengi Ujerumani watashangaa kusikia kwamba wakimbizi waliorudishwa makwao katika hali hii wanaweza kurudi nchini. Seehofer ameshaweka wazi kitisho chake ikiwa itatokea Kansela Merkel ameshindwa kupata mwafaka katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya kuhusu kupokewa wakimbizi waliosajiliwa. Kwa hivyo bado njia ni ndefu ya kuuamua mvutano wa madaraka katika muungano.
Gazeti la «Hannoversche Allgemeine linasema
Ikiwa chama cha Christian Social Union mwishowe kitaamua kuchukua mwelekeo wa peke yake kitaifa, bila shaka hilo litatowa ishara mbaya barani Ulaya. Daima Ujerumani imekuwa na dhima kubwa barani Ulaya kuliko nchi nyingine yoyote kubwa katika Umoja wa Ulaya. Ujerumani ndiyo iliyokuwa kinara wa muungano wa Ulaya na kwa hivyo Ujerumani inabeba sehemu kubwa ya utambulisho wake mpya. Utambulisho huo katika Umoja wa Ulaya kwa wajerumani wengi wanahisi ni mkubwa na wenye uhalisia.
Gazeti la «Donaukurier» linazungumzia juu ya kukamatwa kwa bosi wa kampuni ya magari ya Audi Rupert Stadler. Kukamatwa kwa Stadler kumeitumbukiza kampuni ya Volkswagen katika mgogoro mkubwa wakati ikipambana kuweka mstari kujiepusha na kadhia hiyo. Kuondoka kwa machungu kwa Stadler ni malipo ya kushindwa kwa kampuni nzima. Ushirikiano zaidi na idara za sheria na msingi mzuri wa ushirikiano wa kufanya kazi ungeweza kuifanya kampuni ya Volkswagen kwenye nafasi yake kuwa katika mahala pazuri. Na hata mwendesha mashitaka wa serikali pengine pia angeweza hapo jana kuzuia mapema athari kubwa zaidi.
Gazeti la Märkische Oderzeitung kutoka Frankfurt kuhusu sera ya Mazingira ya Ujerumani.
Sera ya Ujerumani kuhusu mazingira iko katika hali mbaya. Na katika hilo wa kubeba lawama sio waziri anayehusika na masuala ya mazingira katika shirikisho Svenja Schulze kutoka chama cha SPD, bali kwa kiasi kikubwa ni mawaziri wenzake kutoka upande wa muungano wanaosimamia uchumi na uchukuzi. Ujerumani haiwezi kufikia malengo yake ya kupunguza utoaji wa gesi chafu kama ilivyotarajiwa.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Josephat Charo