1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sera za mageuzi katika Umoja wa Mataifa tishio kwa utekelezaji wa maazimio ya malengo ya maendeleo

Epiphania Buzizi3 Agosti 2005

Mageuzi ndani ya Umoja wa mataifa suala ambalo kwa sasa linashughulikiwa zaidi na umoja huo, linapelekea hofu kwamba Mkutano wa kilele juu ya maazimio ya malengo ya maendeleo ya milenia, hautatoa kipaumbele kwa moja wapo ya malengo makuu ya mpango wa mkakati wa kutokomeza janga la njaa na umaskini ifikapo mwaka wa 2015.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi AnnanPicha: AP

Masuala yanayohusiana na maendeleo yamewekwa kando zaidi, kwa sababu ya mtazamo uliopo sasa kwamba mwafaka umekwishafikiwa juu ya mambo yote yanayohusiana na malengo ya maendeleo ya milenia, na kwamba hakuna majadiliano zaidi yanayohitajika.

Afisa wa shirika moja lisilo la kiserikali ambalo huchunguza utendaji kazi wa Umoja wa Mataifa, amebainisha kuwa jukumu la Umoja huo lilikuwa kutathimini mafanikio na matatizo katika kutekeleza maazimio ya malengo ya maendeleo ya milenia ambayo yalipitishwa mwezi Oktoba mwaka wa 2000.

Lakini kwa kuangalia tu kile kinachoendelea kwa sasa, mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa huenda ukaishia kujadili masuala ya kulinda amani, ughaidi, haki za binadamu na mageuzi katika baraza la usalama la umoja wa mataifa, bila kuzingatia kutokomeza umaskini na njaa. Amasema hayo Saradha Iyer, wa shirika hilo lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu nchini Malaysia.

Bi. Iyer, amebainisha kuwa Umoja wa Mataifa unapaswa kutilia mkazo masuala nyeti ya misaada ya kiutu na kutatua migogoro ya dharura, na kuyaacha masuala ya usalama na ugaidi kushughulikiwa na mataifa tajiri ambayo yanajua zaidi nini la kufanya juu ya masuala hayo.

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa ambao utajadili maazimio ya malengo ya milenia, ulielezewa na katibu mkuu wa Umoja huo Kofi Annan kama mkutano muhimu na mkubwa katika historia ya miaka 60 ya umoja huo.

Mkutano huo umepangwa kufanyika kuanzia tarehe 14 hadi 16 mwezi Septemba, na utahudhuriwa na wakuu wa nchi 122, wakuu wa serikali 55 pamoja na mawaziri wa mambo ya nje 13 na maafisa wengine wa serikali.

Wakati huo huo afisa kutoka shirika la kimataifa la Oxfam amebainisha kuwa shirika hilo linahofia kwamba mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa ,utashindwa kuleta maendeleo kwa mataifa yanayokabiliwa na umaskini na ambayo yanahitaji msaada, ikiwa mkutano huo utashindwa kutekeleza angalau baadhi ya maazimio ya Umoja wa mataifa kuhusu maendeleo ya milenia.

Kwa mujibu wa afisa huyo wa shirika la kimataifa la Oxfam, Bi Nicola Reindorp,mambo muhimu ambayo yanapaswa kushughulikiwa na umoja wa mataifa yamaetengwa katika makundi makuu manne ikiwa ni pamoja na kutekeleza maazimio ya maendeleo ya milenia,kuwalinda raia katika maeneo yenye mizozo,kupitisha mikataba kuhusu silaha na biashara pamoja na kuunda mbinu mpya za kuingilia kati pale yanapotokea maafa ya kibinadamu.

Kwake yeye Bi. Reindorp, mkutano wa kilele wa Umoja wa mataifa juu ya maazimio ya maendeleo ya milenia, ni fursa muhimu ya kuhakikisha kuwa miaka 10 pekee iliyobaki katika kipindi cha kutekeleza maazimio hayo kinatumiwa vizuri. Amesema viongozi wa Dunia, hawana budi kuwa na mwamko mpya wa utashi ili kuweza kufanikisha maazimio hayo.

Malengo ya maendeleo ya milenia yanahusu kupunguza umaskini na njaa kwa asilimia 50, kutoa elimu ya msingi kwa wote,kupunguza vifo vya watoto wadogo kwa theruthi mbili, kupunguza robo tatu ya vifo vya wazazi wakati wa kujifungua,kuboresha usawa wa jinsia zote, kudhibiti kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya HIV na UKIMWI,malaria na magonjwa mengine, na vile vile kuweka ushirika wa kimaendeleo kati ya mataifa tajiri na maskini.

Lakini kimsingi utekelezaji wake, umekuwa ukitegemea ongezeko la misada ya kimaendeleo kutoka mataifa wafadhili ya Magharibi.

Mkutano ujao wa kilele,hautatathimini tu mafanikio yaliyokwishapatikana katika utekelezaji wa maazimio ya malengo ya maendeleo ya milenia, bali pia utaweka agenda ya maendeleo kwa miaka mingine kumi inayokuja.

Hata hivyo utekelezaji wa maazimio mengi bado ni ndoto tupu katika maeneo mbali mbali Duniani. Ripoti iliyotolewa na shirika la Kimataifa la Oxfam mwezi uliopita, inabainisha kuwa azma ya kumaliza tofauti iliyopo ya idadi ya watoto wa kike na wa kiume katika shule za msingi imeshindwa kutekelezwa.

Bara la Afrika ambalo masuala yake ya kiuchumi yanatarajiwa kujadiliwa katika mkutano wa kilele wa umoja wa mataiafa,huenda pia likaathiriwa na hali ya sasa ya mambo yaliyopewa kipaumbele na umoja huo, yakiwemo mageuzi katika umoja wa mataifa hususan suala la kuongeza idadi ya nchi zenye viti vya kudumu katika baraza la usalama la umoja wa mataifa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW