1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serbia na Kosovo wasaini makubaliano ya kihistoria

20 Aprili 2013

Viongozi wa Serbia na Kosovo wamesaini makubaliano ya kihistoria Ijumaa (19.04.2013) ya kuwa na uhusiano wa kawaida kati ya nchi hizo mbili hatua ambayo ni muhimu kwa mustakbali wa nchi hizo za Balkan ya Magharibi.

Makubaliano ya Serbia na Kosovo.
Makubaliano ya Serbia na Kosovo.Picha: picture-alliance/AP

Waziri Mkuu wa Serbia Ivica Dacic na mwenzake wa Kosovo Hashim Thaci wametia saini makubaliano hayo yenye vipengele 15 yaliopongezwa duniani kote kufuatia miaka miwili ya mazungumzo magumu yenye nia ya kupunguza mvutano baina ya nchi hizo.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton amesema kile wanachokishuhudia ni hatua ya kuondokana na yaliyopita na ni hatua ya kusonga mbele kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Matumaini yalioko ni kwamba makubaliano hayo yatabadili ukurasa wa eneo la mwisho lenye vurugu katika maeneo ya nchi za Balkan barani Ulaya ikiwa ni miaka 14 baada ya kumalizika kwa vita na miaka mitano baada ya Kosovo kujitangazia uhuru kutoka Serbia.

Thaci amesema kwamba makubaliano hayo yatasaidia kuponya vidonda vya kale na kwamba yanawakilisha enzi mpya ya upatanishi na ushirikiano baina ya mataifa mawili.

(Kutoka kushoto kwenda kulia) Waziri Mkuu wa Serbia Ivica Dacic,Mkuu wa Sera za Kigeni Catherine Ashton, Naibu Katibu Mkuu wa NATO Alexander Vershbow na Waziri Mkuu Hashim Thaci wakiwa katika makao makuu ya NATO mjini Brussels tarehe 19 April 2013.Picha: REUTERS

Naye Dacic akizungumzia makubaliano hayo amesema amewasilisha mapendekezo ya Serbia na kwamba pande zote mbili zitayajadili katika siku zinazokuja kusema wameyakubali au la.

Makubaliano yapongezwa

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameyakaribisha makubaliano hayo na kuzitaka pande zote mbili kutekeleza kwa haraka vifungu vyote vya makubaliano.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema alikuwa akitaka kuzipa hongera na kuzipongeza pande zote mbili kwa msimamo wao imara na kutaraji makubaliano hayo yataleta mustakbali mwema na utulivu katika kanda hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki -moon.Picha: picture-alliance/AP

Waziri wa mambo ya nje wa Austria Michael Spindelegger amesema makubaliano hayo ni ushindi kwa wote.

Lakini katika mji wa kaskazini wa Kosovo wa Kosovska Mitrovisca,Waserbia wa Kosovo wametowa wito wa kuitishwa kwa kura ya maoni na kuyaita makubaliano hayo kuwa ni kusalimu amri na usailiti wa mwisho kuwahi kufanywa na serikali ya Serbia.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kurahisisha njia kwa pande zote mbili katika juhudi za kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Serikali ya Serbia inatarajia kujulishwa tarehe ya kuanza mazungumzo ya kutaka kujiunga na umoja huo katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya hapo mwezi wa Juni na ingelikuwa makubaliano hayo hayangelifikiwa kufikia Jumatatu mipango yake hiyo ingelicheleweshwa kwa muda usiojulikana.

Serikali ya Kosovo bado inatakiwa itambuliwe na mataifa matano kati ya 27 ya Umoja wa Ulaya lakini wakati huo huo kuna matumaini ya kutuzwa kwa kurekebisha tofauti zao na serikali ya Serbia kwa kusaini mkataba wa kabla ya kuanza mazungumzo ya kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya jambo ambalo pia limepangwa kutangazwa katika Mkutano wa Kilele wa mwezi wa Juni.

Taifa ndani ya taifa

Wakati mazungumzo hayo ya miaka miwili yalifanikiwa kupiga hatua kubwa yalikuja kb#ukwama kutokana na suala la hatima ya Waserbia 40,000 walioko kaskazini mwa Kosovo ambao waligoma kutambua mamlaka ya Kosovo na badala yake kuunda taasisi zake wenyewe.

Vikosi vya Usalama vya Kosovo vikiadhimisha miaka mitano ya kujitangazia uhuru kutoka Serbia.Picha: Reuters

Serbia ilikuwa ikiitaka Kosovo ikubali kutawanya madaraka kwa serikali za mitaa za Serbia katika eneo hilo la kaskazini kwa kuwa na polisi yao yenyewe na mahakama zao ili kuhakikisha kwamba watu wa kabila la Waserbia wanakuwa na uwakilishi wa haki nchini Kosovo.

Lakini serikali ya Kosovo ilikuwa na wasi wasi wa kungiliwa kati na serikali ya Serbia katika masuala ya Kosovo kwa kupitia jamii ya Serbia na kwa hiyo kugoma kukubali kuwepo kwa "taifa ndani taifa" katika eneo lake la kaskazini.

Yaliokubaliwa

Kwa mujibu wa makubaliano hayo yaliochapishwa na gazeti litolewalo kila siku nchini Kosovo la Express Waserbia wa Kosovo watapewa nyadhifa fulani za serikali.

Doria ya kikosi cha NATO -KFOR katika mji wa kaskazini wa Mitrovica nchini Kosovo.Picha: DW

Mserbia wa Kosovo atachaguliwa kuwa kamanda wa polisi wa mkoa lakini atakuwa anafuata maagizo kutoka wizara ya mambo ya ndani ya Kosovo ilioko mjini Pristina.

Majaji wa kabila la Waserbia watasimamia mahakama na kutowa hukumu katika masuala mengine ya kisheria kwenye maeneo yanayokaliwa na Waserbia wengi lakini kwa kufuata mfumo wa sheria wa serikali ya Kosovo.

Jumuiya ya Kujihami ya NATO iliingilia kati katika jimbo lililojitenga la Kosovo hapo mwaka 1999 kulazimisha kuondoka kwa vikosi vya Serbia ambapo baadae iliunda kikosi cha KFOR ambacho hivi sasa kimepunguzwa na kuwa na wanajeshi 5,000 kuhakisha usalama.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri:Caro Robi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW