1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Serbia yaahidi kuendelea kuiunga mkono Urusi

4 Septemba 2024

Rais wa Urusi Vladimir Putin amekutana na Naibu Waziri Mkuu wa Serbia Aleksander Vulin Jumatano hii pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Jukwaa la Kiuchumi kwa Mataifa ya Mashariki mjini Vladistock.

Mongolia Ulaanbaatar | Vladimir Putin, Rais wa Urusi
Rais Vladimir Putin amekutana na Naibu Waziri Mkuu wa Serbia Aleksander Vulin baada ya ziara yake fupi nchini Mongolia. Vulin ameahidi kuendelea kuiunga mkono UrusiPicha: Vyacheslav Prokofyev/Sputnik/REUTERS

Rais Putin amekutana na Vulin akitokea ziarani nchini Mongolia. Kwenye mkutano huo, Rais Putin amesikika akimwambia kiongozi huyo kwamba Urusi imemwalika Rais wa Serbia Aleksander Vucic kuhudhuria mkutano wa kilele wa wa kundi la mataifa tajiri na yanayoinukia kiuchumi BRICS, mwezi Oktoba.

Vulin kwa upande wake amesema Serbia sio tu mshirika wa Urusi bali pia ni mshirika wa kimkakati, na kuongeza kuwa hali hiyo imewaongezea shinikizo kutoka mataifa ya Magharibi.

"Serbia, chini ya uongozi wa Aleksandar Vucic ni Serbia ambayo haitawahi kuwa mwanachama wa NATO ambayo haitaiwekea vikwazoUrusi, na haitaruhusu hatua zozote za kupinga Urusi kutekelezwa kutokea eneo lake."

Serbia na Urusi zina mahusiano ya kihistoria na imeendelea kutoiunga mkono Ulaya kuiwekea vikwazo Urusi kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine.

Aleksander Vulin akizungumza na waandishi wa habari. Kiongozi huyu wa Serbia amesema taifa hilo halitakubali kuigeuka Urusi kutokana na shinikizo la magharibiPicha: Marinko Sekulic/DW

Vulin mwenyewe kwa muda mrefu amekuwa mmoja wa waungaji mkono wakubwa wa Kremlin na aliwekewa vikwazo na Marekani mwaka 2023 kutokana na madai ya ufisadi alipokuwa mkuu wa idara za ujasusi nchini humo.

Mkutano huo unafanyika mara baada ya makubaliano makubwa ya kijeshi kati ya Serbia na Ufaransa wiki iliyopita, ambapo Belgrade ilinunua ndege 12 za kivita chapa Rafale. Ndege hizo zitaisaidia kuimarisha jeshi lake la anga na kuziondoa zile za tangu enzi ya Kisovieti.

Katika hatua nyingine, Putin amesema anamtarajia Rais wa China Xi Jinping kuhudhuria mkutano wa kilele wa kundi la mataifa tajiri na yanayoinukia kiuchumi BRICS nchini Urusi mwezi ujao.

Amesema hayo alipokutana na Makamu wa Rais wa China Han Zheng, pembezoni mwa kongamano hilo la mjini Vladistock.

Putin amekuwa akisaka uungwaji mkono wa Xi tangu mzozo kati yake na Ukraine ulipoanza, huku mataifa hayo pia yakiimarisha ushirika wa kibiashara, katikati ya vikwazo vikali vya kiuchumi vya magharibi dhidi ya Urusi.

Mbali na hayo, shirika la habari la Urusi, TASS, limeripoti kuwa ujumbe wa Taliban kutoka nchini Afghanistan umefanya ziara kwenye Jukwaa hilo la Kiuchumi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW