Serengeti - Safari kuelekea kusikojulikana
15 Aprili 2014“Serengeti haitakufa“ – Filamu ya Bernhard Grzimek iliyoshinda tuzo ya Oscar haikuiweka tu Seregenti katika ramani, bali pia iliikuwa kama kioo cha maisha ya porini. Zaidi ya miaka 50 baadaye, mada zilizogusiwa katika filamu hiyo zina umuhimu kuliko ilivyowahi kutokea: Mabadiliko ya tabianchi, ujangili, magonjwa ya wanyama, na ongezeko kubwa la watu vinaitishia tunu hii. Serengeti iko hatarini.
Hata katika safari yake ya kwanza barani Afrika, Bernhard Grzimek alishtushwa na hali ya wanyamapori wa bara hili: “Dunia inazidi kuwa ndogo kwa ajili ya kulisha idadi kubwa na inayozidi kuongezeka ya watu. Hiyo ndiyo sababu idadi ya wanyama inapungua.” Mapema miaka ya 1950, mtafiti huyo wa wanyama alitambua tatizo kuu katika mbuga ya Serengeti: Kadiri idadi ya watu inavyozidi kuwa kubwa, ndivyo inavyozidi kuwa vigumu kuendeleza hali ya kuishi kwa kustahmiliana kati ya binaadamu na mazingira asili.
Wakati huo ni wachache sana katika taifa hilo lililokuwa koloni la Ujerumani katika Afrika ya Mashariki waliokuwa wanajihusisha na utunzaji wa mazingira ya asili. Tayari mbuga ya Taifa ya Serenegeti ilikuwepo, lakini mipaka yake ilikuwa karibu kubadilishwa. Grzimek aliiona hatua hiyo kama kitisho kwa wanyama katika mbuga hiyo. Lakini ni maeneo yapi yalikuwa muhimu hasa kwa wanyamapori? Grzimek na mtoto wake waliamua kuwahesabu wanyama kutokea angani – kwa ufanisi. Walimshawishi rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, juu ya umuhimu wa savana ya kaskazini mwa taifa hilo changa. Utunzaji wa Serengeti uliboreka, shukurani kwa kina Grzimek.
Leo warithi wao wanaisimamia mbuga hiyo ya taifa. Timu ya Afrika ya Jumuiya ya Kutunza Wanyama ya Frankfurt (FZS) inatoa kipaumbele cha juu kabisa kwa mbuga ya wanyama ya Serenegeti. Na leo hii, Serengeti ni miongoni mwa mbuga za wanyama zenye ulinzi bora zaidi duniani. Lakini maisha ya wanyamapori huko yanazihisi athari za ulimwengu wa kisasa. Hiyo inatoa changamoto kwa watunzaji wa wanyama. Kwa mfano, jumuiya ya FZS iliweza kuzuwia ujenzi wa barabara kuu kupitia katika mbuga hiyo. Barabara hiyo ingeweza kuvuruga uhamaji wa wanyama na kuharibu mfumo wa ikolojia wa Seregenti katika muundo wake wa sasa.
Mbuga hii hufadhiliwa kwa kiasi kikubwa kupitia malipo yanayotozwa kwa wageni. Kiasi kingine cha euro milioni moja kutoka mjini Frankfurt kila mwaka, hutumiwa katika ulinzi wa Serengeti. FZS inatumia fedha hizo kuisaidia Mamlaka ya Mbuga za Wanyamapori ya Tanzania (TANAPA) katika programu zake za mafunzo na uendeshaji, au kuipatia vifa vya ufundi kama vile magari yanayotumiwa na wasimamizi wa mbuga. Bila ushirikiano huu na kujitolea bila kuchoka kwa wahifadhi, wanyama wa Serengeti wangekabiliwa tena na maangamizi.
Mwandishi: Inga Sieg
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Kamera na Picha: Axel Warnstedt
Sauti: Moritz Polomski
Uhariri: Klaudia Begic