Sergio Aguero astaafu
15 Desemba 2021Aguero amefikia mwisho wa kusakata kabumbu akiwa Barcelona lakini atakumbukwa daima kwa kuisaidia Machester City kubeba taji la Ligi ya Kuu mwaka 2012.
Mshambuliaji huyo ametangaza kustaafu akiwa na umri wa miaka 33 baada ya kugudulika kwamba ana tatizo la moyo. Aguero aliichezea City kwa muongo mmoja kabla ya kuondoka msimu uliopita akiwa mfungaji bora kwa kutia kimyani mabao 260 katika mechi 400 alizojumuishwa katika kikosi cha timu hiyo.
soma Man City yatawazwa ubingwa wa PL
Lakini bao moja litaendelea kuwa la kihistoria kuliko yote. Mei 13, 2012 Chini ya Kocha Roberto Mancini Manchester City, walishuka dimbani kwa mechi ya fainali ya ligi kuu kama vinara wa ligi pointi sawa na wapinzani wao Manchester United lakini waliwazidi kwa mabao.
United siku hiyo waliifunga Sunderland bao 1-0 wakati City ikifungwa mabao 2-1 na Queen Park Rangers kufikia dakika ya 90 ya mchezo. Lakini kabla ya firimbi ya mwisho Edin Dzeko aliisawazishia City na hatimaye Sergio Aguero dakika ya 93.20 alipachika wavuni bao la tatu na ushindi kwa Manchester City.
Aguero alijiunga na City akitokea Athletico Madrid mwaka 2011. Manchester City wametangaza kwamba watajenga sanamu ya kumuenzi mshambuliaji huyo raia wa Argentina.
Mwezi Mei Aguero alisaini mkataba wa miaka miwili na Barcelona na kukavutia matumaini ya kujumuika na rafiki yake Messi lakini hilo halikuwezekana.
Messi aliihama Barcelona na kuelekea Paris Saint-Germain mwezi Agosti, na Aguero kutokana na jeraha hakuonekana katika mechi za Bercelona hadi Oktoba. Amecheza mechi tano pekee kabla ya kupelekwa hospitali baada ya kuwa na matatizo ya kupumua katika mechi dhidi ya Alaves Oktoba 30 ambapo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu aligundulika kuwa na tatizo la moyo.
AFP