1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wazee wasiojiweza wa Kenya kupokea fedha za usaidizi

Mjahida 28 Januari 2015

Kenya imezindua mpango mpya wa malipo kwa wasiojiweza ambao utawawezesha wazee kupokea takriban dola 25 Kila mwezi kutoka Serikalini.

Baadhi ya wazee wa Kenya
Baadhi ya wazee wa KenyaPicha: picture-alliance/ EPA/D. Kurokawa

Mpango huo umezinduliwa kwenye kongamano la wiki moja la Mpango wa Malipo ya wasiojiweza linaloshirikisha mashirika ya utoaji huduma za jamii kama vile Hazina ya Malipo ya Uzeeni na Bima ya Kitaifa ya Afya.

Mpango huo umezinduliwa wakati ambapo asilimia 46 ya Wakenya wanaishi katika hali ya umasiki licha ya ukuaji wa uchumi wa zaidi ya asilimia 5 miaka miwili iliyopita. Akizindua mpango huo siku ya Jumanne mjini Nairobi, rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema mpango huo kwa jina "Inua Jamii" umenuiwa kuiimarisha jamii ya wazee kwa kiasi kikubwa.

Rais Uhuru KenyattaPicha: Getty Images/AFP/S. Maina

“Hatua zetu za malipo ya kijamii zinalenga watu wachache na ukuaji wa uchumi wetu haujaweza kumaliza umasikini, tayari tumeanza kufanyia marekebisho Hazina ya Kitaifa ya Afya iwe Bima ya Kitaifa ya Afya ili kila mmoja wetu aweze kupata huduma bora za afya kama ilivyo kwenye kifungu nambari 42 cha katiba yetu,”alisema Rais Kenyatta.

Wale watakaofaidika ni pamoja na wazee 164,000 kuanzia miaka 65 wanaoishi katika hali ya umasikini, watu walio na ulemavu wapatao 27,000, na watoto yatima 253,000 na zaidi ya nyumba 10,000 watakaopokea msaada wa vyakula katika maeneo ya mijini. Wote hawa watakuwa wakipokea dola 25 kila mwezi. Hata hivyo wazee wamekuwa wakilalama juu ya fedha hizo kwamba ni kidogo kwa mahitaji yao.

Kiwango kuongezeka

Kwa upande wake Waziri wa kazi wa Kenya Kazungu Kambi, ambaye wizara yake ndio itakayoshughulikia malipo hayo amesema kuna mipango ya kuongeza zaidi fedha hizo ili ziweze kukidhi mahitaji ya watu.

Mkutano huo wa siku nne unaofanyika KICC ulioanza hapo jana, umewaleta pamoja washika dau mbali mbali wote kutoka nchini Kenya na Kimataifa katika harakati za pamoja za kuinua jamii. Mkutano huo pia unatarajiwa kuazisha mpango wa kitaifa utakaotekelezwa na wanachama wote walio katika sekta ya ulinzi wa jamii ili kusaidia katika utoaji wa huduma bora.

Wakenya wakishikilia picha ya rais Uhuru KenyattaPicha: Reuters/Noor Khamis

Aidha benki ya dunia ambayo ni moja ya wafadhili wa mpango huo wa inua jamii, mkuregenzi wake nchini Kenya Diarietou Gayeamesema mpango huu utasaidia kuimarisha uwajibikaji na ukuaji wa mipango zaidi ya jamii.

“Huu ni mpango wa kwanza wa malipo ya wasiojiweza katika jamii wa aina yake duniani kuungwa mkono kwa aina hii na wa kwanza kutekelezwa nchini Kenya. Juhudi hizi zimesaidia kuimarisha maongozi na uwajibikaji na pia kuongeza ukuaji wa mipango kama hii,” alisema bibi Gaye.

Hata hivyo mpango huu unatarajiwa kutekelezwa kwa njia ya elektroniki ambapo kila anayetarajiwa kupokea fedha hizo atasajiliwa kwa njia hiyo na kupema kadi maalumu ilio na alama zao za vidole zitakazowawezesha kupokea malipo kila mwezi. Serikali ya Kenya imetoa shilingi bilioni 1.3 kwa mpango huo huku ikiahidi kuongeza kiwango cha ufadhili kwa mpango huo miaka ijayo

Mwandishi Amina Abubakar/Alfred Kiti
Mhariri Iddi Ssessanga