Serikali mpya ya Italia magazetini
29 Aprili 2013Tuanzie lakini Roma ambako serikali mpya imeundwa miezi miwili baada ya uchaguzi mkuu.Ni serikali ya kwanza ya muunganmo wa vyama vya kihafidhina na mrengo wa shoto tangu mwaka 1947.Wakati waziri mkuu Enrico Letta na mawaziri wake wanakula kiapo cha kuheshimu katiba,katika kasri la rais,risasi zimefyetuliwa nje ya makao makuu ya serikali.Gazeti la "Dresdner Neueste Nachrichten" linaandika:
Ingekuwa risasi hazikufyetuliwa karibu na makao makuu ya serikali,mtu angeweza kuamini kwamba hali ya kawaida ya kimaisha imerejea nchini Italia.Ilidhihirika hatimae kana kwamba vyama vyote viwili vikuu-chama cha mrengo wa shoto cha Democratic-PD na kile cha mrengo wa kulia cha Umma huru-PdL,vimetambua ukweli wa mambo na kutokana na ukosefu wa chaguo mbadala,wameridhia kuunda serikali ya muungano.Lakini hata bila ya risasi kufyetuliwa,serikali hii mpya haionyeshi kutulia-kwasababu inagubikwa na kivuli kisicho cha kawaida cha Silvio Berlusconi.
Maoni sawa na hayo yametolewa na gazeti la "Westfälische Nachrichten" linaloandika:
Enrico Letta si wakuonewa wivu.Kwasababu mivutano ya kuania madaraka haijamalizika.Nyadhifa 21 amebidi kuzigawa sawa bin sawa ili kuridhisha makundi ya mrengo wa shoto na wa kulia katika serikali mpya ya muungano.Vichocheo visipuuzwe katika serikali hii mpya.Hata hivyo kwa kuteuliwa Enrico Letto,serikali safari hii inaongozwa na mwanasiasa na sio tena msomi.Pengine hilo likasaidia kuleta utulivu katika kinyang'anyiro cha kupigania madaraka.
Walinzi wa mazingira wamekomaa
Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha pia na mkutano mkuu wa walinzi wa mazingira mjini Berlin uliowaleta pamoja wawakilishi zaidi ya 800.Gazeti la "Freie Presse" linaandika:
Walinzi wa mazingira wametoa ishara ya mshikamano.Ni nadra kushuhudiwa hali ya usuluhivu katika mkutano mkuu -licha ya mapendekezo 2600 yaliyobidi kufanyiwa marekebisho.Na kwamba mkakati wa uchaguzi unaidhinishwa bila ya kupingwa na hata sauti moja-hilo pia linatajwa kuwa ni maajabu.Chama hicho cha walinzi wa mazingira ambacho kawaida hujulikana kama chama cha wanaopenda kubisha ,kinaonyesha kinaweza kuwatanabahisha wafuasi wake,miaka 30 tangu kilipoundwa,wamedhamiria nini:kutwaa hatamu za uongozi mjini Berlin.Chama cha walinzi wa mazingira kimeshawagutua wafuasi wake,kama watagutuka september 22 ijayo,hakuna ajuaye.
Mada yetu ya mwisho inahusu mtindo wa kupendeleana ndani ya chama cha CSU.Gazeti la "Emder Zeitung" linazungumzia kisa kipya kilichofichuliwa hivi karibuni.Gazeti linaandika:
Wanasiasa wawe mfano wa kuigiza
Wiki iliyopita ilifichuliwa kadhia ya mishahara mikubwa mikubwa kati ya kiongozi wa chama cha CSU katika bunge la Bavaria,Georg Schmidt na mkewe,na sasa ni naibu katibu mkuu wa chama hicho hicho cha CSU Dorothea Bär aliyeingia mashakani.Ndo kusema hakuna vyengine?Hakuna ajuaye.Baada ya kisa cha waziri wa zamani wa ulinzi Karl Theodor zu Gutternberg na mwanasiasa wa bunge la Ulaya Silvana Koch -Mehrin,kughushi shahada za uzamili,ikafuatiwa na madai ya mapendeleo ya aliyekuwa rais wa shirikisho Christian Wulff,watu wanajiuliza kama wanasiasa wanastahiki kuangaliwa kama mfano mwema wa kuigizwa katika jamii.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir(Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman