1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SERIKALI MPYA YA UFARANSA NA HUKUMU YA MICHAIL CHODORKOWSKI

1 Juni 2005

Tuanzie na baraza jipya la mawaziri nchini Ufaransa kufuatia kura ya maoni juu ya katiba ya Ulaya,gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG limechambua athari zinazotokana na mkasa nchini Ufaransa kwa siasa mjini Berlin.Laandika :

„Kwa vyama vya upinzani vinavyojiandaa kushika madaraka mjini Berlin,mwenyekiti wa chama –tawala cha UMP Sarkozy,angekua mtu barabara kushika wadhifa wa waziri mkuu.Sasa lakini upinzani Ujerumani unapaswa kuyaangalia matokeo nchini Ufaransa kwa hisia tofauti.

Mjini Paris serikali ya wahafidhina miaka michache tu baada ya ushindi mkuu ilianza kupoteza imani ya wapigakura.Inaonesha jinsi haraka namna gani imani inavyoweza kutoweka.“-

Likichambua hotuba ya rais wa Israel Mosche Katzav katika Bundestag-Bunge la Ujerumani-gazeti la Süddeutsche Zeitung laandika:

„Shina la hotuba yake ni kifungu hiki cha maneno:“msielewe nisemayo ni maneno ya anaehubiri uadilifu.“ Katzav aliwataka wajerumani kuvaa njuga kupambana barabara na ukweli wa kisiasa juu ya Israel.

Pamoja na ukweli huo wa kisiasa ni mzozo wa Mashariki ya Kati ,kitisho kwa dola la Israel kiliopo miongo kadhaa na pia kutoelewa kanuni za kupunguza mivutano.Risala ya rais Katsav inatoa darasa kwamba desturi pekee hazitoshi kuseleleza uhusiano.Kwa risala hiyo,Ujerumani yafaa kuonesha shukurani.“

Ama gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCHAU juu ya mada hii hii laandika:

„Hotuba ya rais Katsav inamurika tena kile ambacho miaka 40 tangu kuanzishwa uhusiano wa kibalozi na Israel hakingetarajiwa kuwa bora: Kuwapo uhusiano wa kikawaida kati ya nchi hizi mbili baada ya yaliopita.

Bila shaka mahusiano baada ya kuhilikishwa wayahudi na kuvunjika kwa mila nyakati za enzi za utawala wa Manazi kati ya Ujerumani na Israel yalikuwa magumu

sana kuliko vile na Ufaransa.Na bila shaka rais Katsav alikuwa na haki kulalamika juu ya kufufuka mno kwa wimbi la manazi-mambo-leo na chuki dhidio ya wayahudi….Hata hivyo, alisema hayo bila hasira na hii inabainisha imani alionayo kwa Ujerumani ya sasa.Katsav aliionyoshea Ujerumani mkono kwendanayo bega kwa bega katika vita vya kupigania ubinadamu.“

Mwishoe, tutupia macho mjini Moscow:Hukumu ya Michael Chodorkowski imechambuliwa hivi na gazeti la LANDESZEITUNG la Lüneburg:

„Aliekutikana jana na hatia sie tu mkuu wa zamani wa kampuni la mafuta la YUKOS Michail Chodorkowski,bali pia dola la Urusi. Mahkama ya watawala wa kidikteta pia ina hatia……………………

Afisa wa zamani wa shirika la ujasusi la Urusi-KGB-Wladmir Putin yupo upande wa wale wanaotetea Kremlin idhibiti mamlaka juu ya viwanda muhimu nchini Russia.“

Mwishoe, gazeti la HANDELSBLATT kutoka Düsseldorf laandika:

„Hukumu aliopitishiwa Chodorkowski ina maana kwamba Russia haikupiga hatua kubwa katika kutoa mamlaka kwa chombo cha tatu cha dola -Mahkama.Serikali au Kremlin haikuamini kumshtaki Chodokorwski kwa makosa hasa pengine aliofanya katika ubinafsishaji wa kampuni la mafuta la YUKOS au kwa ajili ya kufilisika kwa Banki yake ya MENATEP-Bank.Hii laiti ingelitokea, kesi yake ingegeuka haraka hukumu ya mtangulizi wake Putin-Boris Jelzin.“