Serikali ya Afghanistan yawaacha huru wafungwa wa Taliban
2 Agosti 2020Idadi jumla ya wafungwa wa kundi la walioachiliwa kutoka jela nchini Afghanistan imefikia wafungwa 4,917, baraza hilo limesema.
Wafungwa hao 317 ni miongoni mwa jumla ya wafungwa wengine 500 wa Taliban ambao rais wa Afghanistan Ashraf Ghani aliamuru waachiliwe huru siku ya Ijumaa kama ishara ya kuonesha nia njema.
Kundi la Taliban bado halijatoa tamko lolote kuhusiana na kuachiwa kwa kundi hilo la hivi sasa la wafungwa.
Hata hivyo, siku ya Ijumaa Ghani alisema kuwa hana "mamlaka" chini ya katiba ya nchi hiyo kuwaachilia huru wafungwa wengine 400 waliobakia walioko katika orodha ya Taliban ya kuachiwa kwasababu wamehusika katika uhalifu mkubwa.
Kusitishwa mapigano
Ameongeza kuwa karibuni ataitisha baraza la mashauriano la Loya Jirga, baraza kuu la wazee wa kikabila , kuamua hatima yao. Kundi hilo la wanamgambo limesema limewaacha huru wafungwa 1,000 ilioahidi kuwaacha huru katika makubaliano na Marekani.
Taliban wametangaza makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano kwa muda wa siku tatu wakati wa sikukuu ya Eid al-Adha kuanzia Ijumaa iliyopita. Serikali ilijiunga na hatua hiyo ya kusitisha mapigano.
Makubaliano ya Taliban na Marekani yanasafisha njia kwa ajili ya kuondolewa majeshi yote ya kigeni kutoka Afghanistan na mabadilishano ya wafungwa kati ya serikali ya Afghanistan na wanamgambo hao. Pia yanasafisha njia kwa ajili ya mazungumzo ya amani baina ya Waafghanistan.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Tatu Karema