Serikali Afrika Kusini yakosolewa vifo mgodini vikifika 60
15 Januari 2025Serikali ya Afrika Kusini inakabiliwa na ukosoaji mkubwa kufuatia vifo vya wachimbaji haramu wasiopungua 60waliokwama chini ya ardhi kwa miezi kadhaa, baada ya polisi kuzingira mgodi kwa lengo la kuwakamata mara watakapojitokeza.
Shughuli ya uokoaji iliyoamriwa na mahakama ilianza Jumatatu, ambapo miili ya wachimbaji waliokufa na manusura 132 waliodhoofika sana walitolewa kutoka mgodini, huku mamia ya wengine wakiripotiwa kubaki umbali wa kilomita 2 chini ya ardhi kwenye mgodi wa dhahabu huko Stilfontein, kilomita 150 kutoka Johannesburg.
Polisi walizuia usambazaji wa chakula na maji kwa wachimbaji hao tangu Agosti, hadi mahakama iliporuhusu misaada ya dharura kupelekwa kwao mnamo Desemba.
Wachimbaji waliopatikana hai walikamatwa mara moja na kushtakiwa kwa makosa kama uhamiaji haramu, kuvamia mali, na uchimbaji haramu wa madini. Wachimbaji wengi walikuwa raia kutoka Msumbiji, Zimbabwe, na Lesotho, huku idadi ndogo wakiwa ni Waafrika Kusini.
Soma pia: Watu kadhaa waokolewa, miili yatolewa shimo la mgodi Afrika Kusini
Serikali ilitetea hatua yake, ikisema operesheni hiyo ilikuwa muhimu ili kudhibiti uchimbaji haramu unaosababisha hasara kubwa ya kifedha kwa taifa na sekta ya madini.
Hata hivyo, chama cha upinzani cha DA kiliitaka serikali kuunda tume huru kuchunguza tukio hilo na kuwawajibisha waliohusika, kikieleza kuwa hali hiyo imezidi kuwa mbaya na polisi walionyesha uzembe mkubwa.
Wakati huo huo, juhudi za uokoaji zinaendelea, zikitumia chombo maalum cha chuma kushusha na kuleta juu manusura pamoja na miili ya wachimbaji waliopoteza maisha.
Soma pia: Afrika 2025: Mapambano ya demokrasia na ukuaji
Wachimbaji haramu, wanaojulikana kama "zama zamas", mara nyingi huingia kwenye migodi iliyofungwa wakitafuta mabaki ya madini huku wengine wakiongozwa na magenge ya kihalifu yanayojihusisha na uchimbaji haramu.
Chama cha DA kiliongeza kuwa, licha ya uhalifu unaoambatana na uchimbaji haramu, wachimbaji wa kiwango cha chini mara nyingi ni watu waliokatishwa tamaa wanaojitahidi kutafuta riziki katika mazingira magumu.