1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Burundi yaunga mkono marekebisho ya katiba

26 Oktoba 2017

Serikali ya Burundi imeidhinisha marekebisho ya katiba ambayo yatatoa fursa ya kurefushwa kwa uongozi wa Rais Pierre Nkurunzinza, kulingana na maelezo ya maafisa waandamizi wa serikali hiyo.

Burundi Pierre Nkurunziza
Picha: picture-alliance/dpa/C. Karaba

Huenda uongozi wa rais Pierre Nkurunzinza ukarefushwa kwa miaka mingine 14. Hii ni baada ya serikali ya Burundi inayokabiliwa na migogoro kuidhinisha marekebisho ya katiba ambayo yatatoa fursa ya kurefushwa kwa uongozi wake, kulingana na maelezo ya viongozi wakuu.

Mawaziri, waliokutana jumanne katika kikao maalumu, waliafiki misingi ya mageuzi yaliopendekezwa.

Katiba ya sasa ya taifa la Burundi inatokana na makubaliano ya amani ya mwaka wa 2000, yaliyosainiwa katika mji wa kaskazini mwa Tanzania wa Arusha ili kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 12 ambayo ilisababisha vifo zaidi ya 300,000.

Kwa mujibu wa afisa ambaye hakutaka jina lake litajwe, mabadiliko yanayopendekezwa hayatagusa viwango vya mgao wa madaraka kwa misingi ya kabila na jinsia, katika serikali, bunge na polisi, lakini hakuna popote makubaliano ya amani ya Arusha yanakotajwa.

Makubaliano ya Arusha yanasema wazi kwamba hakuna rais anayeweza kutawala nchi kwa zaidi ya miaka 10.

Lakini Burundi inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa, uliochochewa wakati makundi ya upinzani, yalipoamua kutetea yaliokubaiwa kwenye mkataba wa Arusha, kwa kupinga uchaguzi mnamo Aprili 2015 ambayo ulimwezesha Nkurunziza kubakia madarakani kwa kipindi chengine cha miaka mitano.

Maafisa wa usalama wakikabiliana na waandamanaji Burundi mnamo Mei 2015Picha: Reuters/G. Tomasevic

Ushindi wa kiongozi huyo wa miaka 53 uliitumbukiza taifa hilo  katika matatizo, na mamia waliuawa katika machafuko yaliyotokea. Karibu watu 400,000 wamekimbia nchi hiyo. Mabadiliko ya katiba yanasema "rais wa jamhuri anachaguliwa kwa muda wa miaka saba ambayo yanaweza kuongezewa" lakini inaongezea, "hakuna rais anaweza kutawala kwa zaidi ya mihula mawili mfululizo."
Kwa nadharia, hii inaweza kumaanisha kwamba Nkurunziza angeweza kuchaguliwa mwaka wa 2020 na kuchaguliwa tena miaka saba baadaye, pamoja inamuongezea muda zaidi wa kuhudumu kwa miaka 14.

Kulingana na duru nyengine,  mawaziri pia walikubaliana kuwa rasimu ya katiba – ambayo ni matokeo ya zoezi la mashauriano yaliyotolewa katika mapendekezo kutoka kwa watu 26,000 inaweza kupigiwa kura ya maoni kwa haraka, na labda huenda ikawa mwezi Februari mwaka ujao.

Mwandishi: Fathiya Omar/AFPE

Mhariri: Gakuba, Daniel