1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Chad yatangaza tahadhari kufuatia kushambuliwa idara nyeti

29 Februari 2024

Vikosi vya usalama vinafanya upekuzi wa jumla wa magari na wapita njia kwenye mji mkuu wa Chad, N'Djamena baada ya milio ya risasi kusikika karibu na makao makuu ya chama kikuu cha upinzani.

Chad N'Djamena | Mandhari ya mtaani
Hali inaonekana kuwa tulivu mjini N'DjamenaPicha: Denis Sassou Gueipeur/AFP/Getty Images

Vikosi vya usalama vinafanya upekuzi wa jumla wa magari na wapita njia kwenye mji mkuu wa Chad, N'Djamena baada ya milio ya risasi kusikika karibu na makao makuu ya chama kikuu cha upinzani cha Socialist Party Without Borders - PSF.

Hii ni baada ya serikali ya Chad kusema kuwa watu kadhaa waliuawa katika shambulizi kwenye ofisi ya idara ya usalama wa ndani na kuwatuhumu wale iliyowataja kuwa wanachama wa upinzani kwa kuhusika na tukio hilo.

Kiongozi wa chama cha PSF, Yaya Dillo na mpinzani mkubwa wa Rais wa Mpito wa Chad, Mahamat Idriss Deby Itno, amekanusha kuhusika katika shambulizi hilo la Jumanne usiku.

Soma pia: Milio ya risasi yasikika mjini Ndjamena

Akizungumza na shirika la habari la Ufaransa, AFP, Dillo ambaye pia ni binamu wa Deby, amezitaja shutuma hizo kama za "uwongo", akisema hakuwepo wakati mkasa huo ukitokea.

Amesema lengo la serikali ni kumzuia, na kumtisha ili asigombee uchaguzi. Shambulizi hilo limefanyika siku moja baada ya kutangazwa kuwa uchaguzi wa Chad utafanyika Mei 6, uchaguzi ambao Deby na Dillo wote wanakusudia kugombea.