Serikali ya chama cha Kiisilamu Tunisia kujiuzulu
29 Septemba 2013Chama hicho kikuu cha wafanyakazi nchini humo kiliitisha mkutano kati ya chama hicho kinachofuata nadharia za dini ya Kiislamu pamoja na upinzani usiopendelea dini kuwa msingi wa maadili ya jamii ili kukubaliana juu ya tarehe wiki ijayo ambapo kutafanyika mjadala wa kitaifa, wenye lengo la kumaliza mzozo uliozushwa na mauaji ya mbunge maarufu wa upande wa upinzani Julai mwaka huu.
Vuguvugu la mapinduzi ya umma
Nchi hiyo ambayo ni chanzo cha vuguvugu la mapinduzi katika mataifa ya Kiarabu mwaka 2011 imetumbukia katika mzozo wa kisiasa , wakati upande wa upinzani usiopendelea dini kuwa msingi wa maadili ya umma ukikishutumu chama cha msimamo wa wastani cha Ennahda kwa kushindwa kuwadhibiti watu wenye itikadi kali ya dini ya Kiislamu.
Katika taarifa iliyochapishwa katika tovuti yake chama hicho cha wafanyakazi cha UGTT, ambacho kimekuwa na uhusiano usiokuwa mzuri na chama cha Ennahda na hapo kabla kukishutumu chama hicho kwa kuburuza miguu katika hatua za mageuzi nchini humo, kimesema kuwa chama hicho tawala kimekubali mpango wake wa mpito.
"Taasisi hiyo inayodhamini mpango huo inakaribisha matokeo hayo na inatoa wito kwa vyama vyote kujiunga na majadiliano ili kuteua tarehe kwa ajili ya mjadala wa kitaifa," kimesema chama hicho, na kuongeza kuwa kinamatumaini ya kuitisha mkutano huo baadaye wiki ijayo. Chama cha wafanyakazi cha UGTT hapo kabla kimetoa wito wa kufanya kampeni ya upinzani kuhakikisha kuwa chama cha Ennahda kinakubaliana kikamilifu na mpango wake huo wa mpito.
Shutuma
Chama hicho kimekishutumu chama cha Ennahda kwa kufanya kila kiwezacho kuhakikisha kushindwa kwa mpango huo, ambao kimeutayarisha pamoja na chama cha waajiri Utica, shirika lisilokuwa la kiserikali la kutetea haki za binadamu nchini humo la Tunisia League for Human Rights , pamoja na chama cha wanasheria.
Ennahda imekataa mabadiliko, na inaushutumu upinzani ambao kwa kiasi kikubwa unapinga dini kuwa msingi wa maadili, kwa kuvuruga mapendekezo ya wapatanishi kwa kudai serikali ijiuzulu mara moja. Mpango huo umeweka muda wa wiki tatu kwa kuundwa baraza la mawaziri litakalokuwa na wajumbe ambao si wanasiasa litakalochukua nafasi ya serikali ya sasa, baada ya kuanzishwa kwa majadiliano na vyama vya upinzani.
Pia limeweka muda wa wiki nne wa kuidhinishwa kwa sheria mpya za uchaguzi, na kuweza muda maalum wa uchaguzi mpya na kukamilisha mswada wa katiba mpya ambao umecheleweshwa kwa muda mrefu. Msemaji wa chama cha Ennahda Lajmi Lourimi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa chama chake "kiko tayari kuingia katika majadiliano na vyama vyote ambavyo vitapenda". "Mjadala wa kitaifa unaweza kuanza wiki ijayo, lakini hakuna tarehe iliyokwisha pangwa."
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Bruce Amani