1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya DRC kuharamia maziko ya 26 walioangamia Kinshasa

3 Februari 2022

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imesema itagharamia mazishi ya wahanga wa ajali ya Matadi Kibala ambapo watu 26 walifariki kutokana na kukatika kebo ya umeme yenye nguvu nyingi katika soko moja mjini Kinshasa

Demokratische Republik Kongo | Mehrere Tote bei Unfall mit Hochspannungsleitung
Picha: Pepele News/REUTERS

Watu 26 waliofariki katika ajali hiyo kwenye soko la Matadi Kibala, wengi wao ni wanawake wachuuzi walionaswa asubuhi na mvua kubwa iliyonyesha kwenye eneo wanakofanyia kazi zao. Ni wakati mvua hiyo ikinyesha ndipo kebo yenye nguvu kubwa za umeme ilipokatika kutoka kwenye nguzo yake na kuangukia kwenye njia iliyokuwa na majimaji ambapo waathiriwa walikuwa wanauza bidhaa zao. Kwa sasa miili yao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya Kinshasa.

Rais Félix Tshisekedi, Waziri Mkuu Jean-Michel Sama Lukonde na viongozi kadhaa walitembelea eneo kulipotokea ajali hiyo. Serikali imesema itasimamia mazishi hayo, kama anavyoeleza waziri mkuu Jean-Michel Sama Lukonde. "Hapa tutachukua kwanza majukumu yetu ya kujihusisha na  mazishi ya watu waliofariki na kwa haraka sana pamoja na viongozi wa mji, tutaangalia jinsi ya kupata suluhisho ya kudumu kwa suala hili la soko la Matadi Kibala".

Hali kweli ni ya masikitiko. Shirika la Umeme hapa nyumbani (SNEL) limeihusisha ajali hiyo na radi iliyopiga nyaya, jambo ambalo wakaazi wengi hawalikubali, wakiamini kuwa msiba umetokea kutokana na kuchakaa kwa nyaya hizo. Huyu hapa mmoja wa wakaazi wa Matadi Kibala ambaye hakutaka jina lake kutotajwa. "Katika wilaya ya Matadi Kibala kuna nguzo mbili za umeme wa Inga ambazo hivi leo mvua ilikuwa kubwa, kebo ilikatika. Kwa kweli, nyaya hii tayari ilikuwa tete".

Upande mwengine, wabunge wa kitaifa wanamlaumu mkurugenzi wa SNEL wakimtaka kujieleza mbele ya bunge. Mbunge Gaël Bussa tayari amewasilisha swali kwenye ofisi ya Bunge la Kitaifa. Kwenye msiba DW ilikutana na mbunge Nsingi Pululu ambaye alisema majukumu yapo kwenye ngazi mbili.

"Ilichukua zaidi ya dakika tano kabla tahadhari kutolewa. Ni la kusikitisha upande wa kiufundi kwani hapo kulikuwa na hitilafu. Halafu upande wa utawala, kuna usimamizi mbovu wa harakati za watu. Yaani, majukumu ni kwenye ngazi hizo mbili na ni hali mbaya. Majukumu yanaonekana wazi".

Ajali hiyo imetokea wiki tatu tu baada ya Rais Félix Tshisekedi kuagiza Baraza la Mawaziri kuhamisha soko la Matadi Kibala.

Mwandishi: Jean Noël Ba-Mweze, DW, Kinshasa. 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW