1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Italia kupigiwa kura ya imani

2 Oktoba 2013

Wakati Bunge la Italia likiandaa kura ya kuwa au kutokuwa na imani na serikali, waziri mkuu wa nchi hiyo Enrico Letta amewatahadharisha wabunge juu ya hatari itakayolikabili taifa, ikiwa wataiondolea imani serikali yake.

General view of the Senate during Italy's Prime Minister Enrico Ukumbi wa baraza la seneti la Italia alikotoa rai yake Enrico Letta
Ukumbi wa baraza la seneti la Italia alikotoa rai yake Enrico LettaPicha: Reuters

Mgogoro uliibuka katika serikali ya Italia baada ya agizo la waziri mkuu wa zamani Silvio Berlusconi kuwataka wanachama 5 wa chama chake kujiondoa katika baraza la mawaziri, kupinga kuondolewa kinga kwake na kuzitisha uwezekano wake kutimuliwa katika baraza la seneti.

Akizungumza bungeni leo muda mfupi kabla ya zoezi la kupiga kura juu ya imani kwa serikali yake, waziri mkuu wa Italia Enrico Letta amesema wataliano wamechoshwa na wanasiasa wanaokabana shingo bila kuleta mabadiliko yoyote, na kuongeza kuwa wananchi hao hawataki kuendelea kuiona hali hiyo.

Turufu mikononi mwa wabunge waasi

Kunusurika kwa serikali yake kunategemea kwa kiasi kikubwa wabunge kutoka chama cha Watu wa Uhuru, PDL cha waziri mkuu wa zamani Silvio Berlusconi, ambao wanatarajiwa kujitenga na msimamo wa bwana Berlusconi, aliyewataka kuiangusha serikali ya sasa kwa kuwaomba wanachama wa chama hicho kujiuzulu kutoka serikalini.

Waziri Mkuu wa Italia Enrico Letta akizungumza bungeni leoPicha: Reuters

Berlusconi ambaye ni tajiri na mmiliki wa vyombo vingi vya habari, amekitaka chama chake kupiga kura ya kutokuwa na imani na serikali.

Katika hotuba bungeni, Letta amesema serikali yake ina mipango kabambe na yenye urari, katika kutekeleza mageuzi katika nchi hiyo inayokabiliwa na mzozo wa kiuchumi. Amesema mpango huo utatekelezwa katika kipindi cha miezi 12.

Enrico Letta ambaye serikali yake imekuwa madarakani kwa muda wa miezo mitano amesema, ''Tupe imani yenu ili tuweze kuyatimiza majukumu haya, tupe imani yenu kuunga mkono yale yote ambayo tumekwishayatekeleza''.

Berlusconi matatani

Kwa upande mwingine, Berlusconi ambaye alieleza bayana kupitia barua yake iliyochapishwa na gazeti la Tempi kwamba ameamua kuiangusha serikali ya bwana Letta, ameonyesha kulegeza msimamo wake leo, alipoingia bungeni.

Waziri mkuu wa zamani wa Italia Silvio Berlusconi aweze kutelekezwa na wabunge wa chama chakePicha: Reuters

''Tutaangalia kile kitakachotokea, tutaisikiliza hotuba ya waziri mkuu Letta, na kisha tutaamua'', amesema Berlusconi, kama alivyokaririwa na vyombo vya habari.

Chama chake cha PDL kinakabiliwa na mgogoro, baada ya uamuzi wa wabunge wa chama hicho na pia washirika wa karibu wa Berlusconi, akiwemo mrithi wake Angelino Alfano, kutamka wazi kwamba wangeiunga mkono serikali.

Mzizi wa fitina katika suala hili ni kura itakayopigwa bungeni siku ya Ijumaa, ambamo bwana Berlusconi anaweza kupoteza kiti chake katika baraza la seneti, kutokana na hukumu ya kifungo cha miaka minne jela, ambacho alipewa baada ya kupatikana na hatia za rushwa.

Sheria ya mwaka 2012 inamzuia mtu yeyote aliyepewa kifungo cha zaidi ya miaka 2, kutumikia ofisi ya umma kwa zaidi ya miaka 6. Berlusconi ameipinga sheria hiyo, na amewashutumu majaji waliomhukumu kifungo jela kuwa na njama ya kumfukuza katika siasa za Italia.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE

Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi